1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya kupinga Uislamu yashamiri

Abdu Said Mtullya9 Desemba 2014

Wahariri wanazungumzia maandamano ya kuupinga Uislamu nchini Ujerumani, mjadala juu ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani na pia wanazungumzia juu ya juhudi za kupambana na umasikini.

https://p.dw.com/p/1E1LG
Wapinga Uislamu. waandamana nchini Ujerumani
Wapinga Uislamu waandamana nchini UjerumaniPicha: Reuters/Hannibal Hanschke

Juu ya maandamano ya kuupinga Uislamu ambayo yamekuwa yanafanyika kwa wiki kadhaa katika miji mbalimbali ya Ujerumani, mhariri wa gazeti la "Badische Neuste Nachrichten" anasema miongoni mwa wanaoshiriki katika maandamano hayo ni wananchi wa tabaka la kati wenye hofu juu ya waislamu wenye itikadi kali wanaokusudia kuleta utawala wa kiislamu nchini Syria na Iraq kwa kutumia njia za ukatili mkubwa.

Mhariri huyo anasema wananchi hao pia wana hofu juu ya kutokea mashambulio ya kigaidi baada ya kurejea nchini Ujerumani kwa waislamu wenye itikadi kali walioenda kujiunga katika vita vya kundi la dola la kiisllamu .Watu hao wanaweza kufanya mashambulio nchini kutokana na hasira na kutamauka.

Mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" anasema wananchi hao wa tabaka la kati wana haki kabisa ya kuwa na hofu na hofu hiyo haiwezi kupuuzwa kwa kutoa miito ya stahamala.

Ukosefu wa stahamala

Lakini mhariri wa gazeti la "Eisenacher Presse" anasema yeyote anaeshiriki katika maandamano hayo anaonyesha jinsi Ujerumani ilivyokuwa na utovu wa stahamala.Mhariri huyo anasema wananchi wenye wasiwasi wanapaswa kuonyesha na kuyatoa maoni yao kwa uwazi. Kwani mtu haonyeshi stahamala kwa kunyamaza kimya.

Maandamano dhidi ya maandamano

Gazeti la "Freie Presse" linatilia maanani kwamba maalfu ya wananchi wengine pia walifanya maandamano ya kuwapinga hao wanaoupinga Uislamu. Mhariri wa gazeti hilo anasema hiyo ni hatua sahihi lakini anashauri maandamano hayo ya kuwakabili wanaopinga Uislamu yafanyike kila siku.

Gazeti la "Die Welt" linatoa maoni maoni juu ya matukio ya hivi karibuni nchini Marekani ambako Wamarekani kadhaa wenye asili ya Afrika wameuliwa na polisi weupe . Mhariri wa gazeti hilo anasema matukio hayo hayatokani na ubaguzi wa rangi bali yanatokana na uhafifu wa mafunzo miongoni mwa polisi.

Mhariri huyo anasema pana haja ya kuleta mageuzi katika jeshi la polisi nchini Marekani. Anasema mfano mzuri umetolewa na polisi wa Rialto katika jimbo la California ambako polisi wanavalishwa kamera miilini. Utaratibu huo umepunguza matumizi ya nguvu miongoni mwa polisi kwa asilimia 60 na pia malalamiko ya wananchi yamepungua kwa asilimia 88. Mhariri wa gazeti la "Die Welt" anaamini kwamba, laiti utaratibu huo wa kamera ungelitumika katika sehemu zote nchini Marekani, Michael Brown,Eric Garner na Tamir Rice bado wangelikuwa hai.

Usawa utaleta ustawi wa uchumi

Wataalamu wa Shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo,OECD wamechapisha mtaala juu ya hali ya umasikini duniani. Juu ya mtaala huo mhariri wa gazeti la "Landeszeitung" anasema,ukweli kwamba tafauti kati ya tajiri na masikini imezidi kuongezeka siyo jambo la kushangaza wala la kuwashtua wanasiasa.Lakini uchunguzi wa wataalamu hao unapaswa kuzifanya serikali zijieleze juu ya suala la umasikini. Katika ripoti yao wataalamu wa OECD wamesema kuwa ustawi madhubuti wa uchumi unaweza kuletwa na kudumishwa ikiwa tu serikali zitachukua hatua za kuziondosha tafauti baina ya tajiri na masikini ambazo zinazidi kuongezeka.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu

LINK: http://www.dw.de/dw/article/0,,18117991,00.html