1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya kuiunga mkono serikali yafanyika Iran

5 Januari 2018

Maandamano ya kuiunga mkono serikali ya Iran yanatarajiwa kufanyika mjini Tehran Ijumaa huku uongozi wa nchi hiyo ukitaka kuyamaliza machafuko yaliyoshuhudiwa wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/2qNza
Iran Proteste pro Regierung in Teheran
Picha: picture-alliance/dpa/E. Noroozi

Haya yanajiri wakati ambapo Marekani imeiwekea Iran vikwazo na kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao maalum kuizungumzia hali ya Iran.

Maafisa wa Iran wametangaza kutakuwepo na maandamano 40 katika sehemu tofauti za mkoa wa Tehran baada ya sala ya Ijumaa, huu ukiwa ni mwendelezo wa maandamano ya kuiunga mkono serikali ambayo yameshuhudiwa katika miji mingine katika kipindi cha siku mbili zilizopita.

Mapema Ijumaa katika barabara za Tehran kulikuwa na idadi kubwa ya maafisa wa polisi ingawa hakukuwa na ripoti za maandamano mapya usiku kucha, lakini zimekuwepo taarifa kwamba kulikuwa na maandamano madogo madogo ya kuipinga serikali katika miji ya mikoa kadhaa. Hata hivyo taarifa hizi hazijaweza kuthibitishwa. Wanaharakati wameweka video katika mitandao ya kijamii kuonesha maandamano hayo ambapo wanasema waandamanaji walikuwa wanayatamka maneno ya kumpinga kiongozi Ayatollah Ali Khamenei.

Marekani imeziwekea vikwazo kampuni tano za Iran

Wanaharakati kadhaa wanaunga mkono maandamano ya kuipinga serikali akiwemo Shirin Ebadi ambaye ni maarufu kwani alishinda tuzo ya Nobel, "maandamano ya amani yanastahili kuendelea ili kuishurutisha serikali ya Iran iwasikilize watu wake," alisema Ebadi, "kwa mfano watu wanastahili kuacha kulipia umeme, maji na gesi. Wanastahili kuacha kulipa kodi na watoe pesa zao katika benki," aliongeza mwanaharakati huyo.

USA Finanzminister Steven Mnuchin im Weißen Haus in Washington
Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin ametangaza vikwazo dhidi ya IranPicha: Getty Images/A. Wong

Wakati huo huo Marekani imeziwekea vikwazo kampuni tano za Iran ambazo zinadaiwa kushughulikia mpango wa silaha za masafa marefu na imesema kwamba hatua hiyo ndiyo mojawapo iliyosababisha maandamano hayo ya Iran.

Waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin amesema vikwazo hivyo vinalenga sehemu muhimu za mpango wa makombora ya masafa marefu wa Iran, ambao serikali inaupa kipau mbele mpango huo kuliko maslahi ya kiuchumi ya raia wa Iran.

Iran kupitia Balozi wake katika Umoja wa Mataifa Gholamali Khoshroo imelalamika kwamba ujumbe wa Rais Donald Trump katika mtandao wa kijamii wa Twitter ndio uliochochea maandamano lakini Marekani imekanusha kuhusika kwa vyovyote katika maandamano hayo ikisema yalitokea ghafla tu.

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamegawika

Hayo yakiarifiwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapanga kufanya kikao kuhusiana na Iran mchana wa Ijumaa baada ya Marekani kuliambia Baraza hilo kuwaunga mkono Wairan wanaoipinga serikali yao kwa kuandamana.

USA Sicherheitsrat der Vereinten Nationen Friedensverhandlungen in Kolumbien
Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa litafanya kikao Ijumaa mchanaPicha: picture-alliance/dpa/M. Rajmil

Huku wanachama wa Baraza hilo wakiwa wamegawika kimaoni kuhusiana na maandamano hayo yaliyolikumba taifa hilo la Kiislamu, haijabainika mazungumzo hayo yatakuwaje au matokeo yake yatakuwa yapi.

Msemaji wa rais wa sasa wa Baraza hilo la Umoja wa Mataifa ambaye ni Afghanistan, Alma Konurbayeva amethibitisha kwamba kikao hicho kitakuwa kuhusu Iran.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE

Mhariri: Gakuba Daniel