Maandamano makubwa yatarajiwa Venezuela | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maandamano makubwa yatarajiwa Venezuela

Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido amewataka wafuasi wake wazidi kuandamana , siku moja baada ya machafuko kuripuka mjini Caracas , na kutajwa na Rais Nicolas Maduro kuwa "njama ya mapinduzi iliyoshindwa".

Juan Guaido anasema maandamano ya leo jumatano yatakuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Venezuela.

 "Navitolea wito vikosi vya jeshi viendelee na "opereshini ya uhuru". Amesema katika risala yake kwa njia ya video kupitia mitandao ya kijamii, kiongozi wa upinzani aliyejitangaza kuwa rais wa mpito wa Venezuela Juan Guaido na kuwahimiza wafuasi wake wote wateremke kwa wingi majiani  kote nchini Venezuela mnamo siku ya leo ya mei mosi.

Hata hivyo rais anaebishwa Nicolas Maduro anaonyesha kutojali wito huo hasa baada ya wito kama huo uliotolewa jana kuwataka wanajeshi waasi, kushindwa kwa sehemu kubwa.

Maduro binafsi anaepanga kuongoza maandamano ya mei mosi leo mjini Caracas, ametangaza ushindi dhidi ya waasi na kuwapongeza wanajeshi kwa kuwashinda nguvu "kundi dogo la waasi waliotaka kueneza matumizi ya nguvu kupitia vijighasia vya waliotaka kufanya mapinduzi.

Magari ya wanajeshi yakiwaandama waandamanaji mjini Caracas

Magari ya wanajeshi yakiwaandama waandamanaji mjini Caracas

Baadhi ya wanajeshi wa Venezuela wamekimbilia katika ubalozi wa Brazil mjini Caracas

Jana waandamanaji wanaomuunga mkono Guaido walipambana na vikosi vya usalama  katika barabara za mji mkuu Caracas. Watu wasiopungua 69 wamejeruhiwa, wawili kati yao kwa risasi.

Akihutubia kupitia televisheni ya taifa jana usiku, rais Nikolas Maduro ameahidi kuwaandama mahakamani wale wote waliokuwa nyuma ya tukio hilo. Amehakikisha serikali yake inadhibiti hali ya mambo na kwamba uongozi wa kijeshi unaendelea kumuunga mkono pamoja na serikali yake.

Rais Maduro amekanusha ripoti ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo aliyesema Maduro alikuwa akijiandaa kukimbilia Cuba kabla ya kuzuwiliwa kuondoka na Urusi.

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuiwekea vikwazo vikali Cuba ikiwa haitoacha kuiunga mkono kijeshi Venezuela.

Wakati huo huo Brazil inasema baadhi ya wanajeshi wa Venezuela wameomba kinga ya ukimbizi katika ubalozi wake mjini Caracas. Vyombo vya habari vya Brazil vinasema idadi yao inafikia wanajeshi 25.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress amezitolea wito pande zote mbili zijiepushe na matumizi ya nguvu.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com