1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano dhidi ya rais Musharraf

21 Septemba 2007

Mamia ya wafuasi wa upinzani nchini Pakistan wameshiriki kwenye maandamano ya kumtaka rais Pervez Musharraf aondoke kutoka madarakani.

https://p.dw.com/p/CH7u
Jenerali Pervez Musharraf
Jenerali Pervez MusharrafPicha: AP

Wakati huo huo wajumbe wa upinzani wamesema kuwa watasusia kikao cha bunge cha tarehe 29 mwezi huu kama hatua ya kupinga azma ya rais Musharraf ya kutaka kugombea tena kiti cha rais.

Uchaguzi wa rais nchini Pakistan unakabiliwa na mwanzo wenye wimbi la misukosuko.

Wafuasi wa upinzani walioandamana wanataka utawala wa jenerali Pervez Musharraf uanguke.

Waandamanaji hao walikusanyika nje ya mahakama kuu mjini Islamabad huku wakipiga mayowe kwamba Musharraf aende, fujo hizo zimetokea siku moja tu baada ya maafisa wa uchaguzi nchini Pakistan kutangaza kuwa jenerali Musharraf atagombea tena wadhfa wa rais kwa kipindi kingine cha miaka mitano katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika tarehe 6 mwezi ujao wa Oktoba.´

Misukosuko hiyo inatokea wakati ambapo jenerali Musharraf amemteuwa Nadeem Taj kuwa mkuu mpya wa shirika la ujasusi.

Taj amemrithi Ashfaq Kiyani ambae anatarajiwa kushika madaraka ya juu ya kijeshi iwapo rais Musharraf atashinda katika uchaguzi na hatimae kutimiza ahadi yake ya kujivua madaraka hayo ya kijeshi.

Maandamano ya leo yaliwashirikisha wafuasi wa muungano vyama vya upinzani vyenye misingi ya kidini, chama cha Muslim League-Nawaz cha waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif ambae alifukuzwa kutoka nchini Pakistan wiki iliyopita mara tu aliporejea kutoka uhamishoni na makundi mengine yanayompinga jenerali Musharraf.

Vyama hivyo vemetishia kuitisha maandamano kote nchini Pakistan ili kumzuia rais Musharraf asichaguliwe kwa mara nyiyngine tena.

Wanasheria waliofaulu kupinga kumrejesha kazini jaji mkuu Iftitikhar Chaudhry wamesema watajikita katika ofisi za tume ya uchaguzi tarehe 29 Septemba wakati stakabadhi za uteuzi wa jenerali Pervez Musharraf zitakapowasilishwa.

Rais wa jopo la mahakama kuu ya Pakistan, Munir Malik na mwanasheria Aitazaz Ahsan aliye muwakilisha jaji mkuu Iftikhar Chaudry wakti wa kesi yake wamesema umoja wa wanasheria utaendeleza juhudi zake kwa amani ili kupinga mpango wa rais Musharraf wa kutaka achaguliwe tena.

Wanasheria nchini Pakistan wameionya serikali iache vitendo vya kutumia nguvu dhidi ya wanasheria, wanahabari na raia kwa jumla.

Mcheza Kriket wa zamani Imran Khan ambae sasa ni mwanasiasa aliwaambia wafuasi wake ambao pia walishiriki kwenye maandamano hayo kwamba rais Musharraf anaikejeli Pakistan mbele ya ulimwengu.

Wakati huo huo takriban waandamanaji 300 walikusanyika na kufanya maandamano katika mji wa kusini wa Karachi, mtu mmoja amekamatwa na polisi.

Vyama vyenye misingi ya kidini na chama cha mwanasiasa Imran Khan vimewasilisha malalamiko mahakamani dhidi ya majukumu mawili ya rais Musharraf kwa wakati mmoja na iwapo kiongozi huyo ana haki ya kugombea tena kiti chake.

Mahakama kuu inatarajiwa kutoa uamuzi wake mapema wiki ijayo.

Upinzani mkali dhidi ya rais Pervez Musharraf katika mwaka huu ulianza tangu pale mbinu yake ya kumfuta kazi jaji mkuu Iftikhar Chaudhry ya mwezi Machi iliposhindwa, hatua hiyo imempunguzia umaarufu jenerali Musharraf kwa kiasi kikubwa hadi kufikia kutangaza kwamba atajiuzulu madaraka yake ya kijeshi.

Jenerali Musharraf amesema kuwa ataapishwa kama raia mara tu muda wake utakapo kamilika hapo tarehe 15 mwezi Novemba japo kuwa kuna tetesi kwamba huenda akaachia madaraka ya kijeshi kabla ya uchaguzi.

Wachambuzi wanasema kuwa rais Musharraf anakuwa makini katika kumteuwa mrithi atakae chukua madaraka ya kijeshi kwa kuchelea asije akakabiliwa na mapinduzi mara atakapokuwa rais wa kiraia.