Maandamano dhidi ya filamu ya kuukashifu Uislamu yasambaa | Matukio ya Afrika | DW | 13.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Maandamano dhidi ya filamu ya kuukashifu Uislamu yasambaa

Maandamano ya Waislamu yameenea sehemu nyingi duniani wakipinga filamu iliyotengenezwa Marekani na inayomkashifu Mtume Muhammad, ambapo polisi wa Cairo wametumia mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji hao.

Maandamano dhidi ya filamu ya kumkashifu Mtume Muhammad mjini Tunis, Tunisia.

Maandamano dhidi ya filamu ya kumkashifu Mtume Muhammad mjini Tunis, Tunisia.

Rais wa Muhammed Mursi wa Misri ametoa baraka za kufanyika kwa maandamano ya amani lakini akasema ni kinyume kuwaua raia na kushambulia balozi. "Kutoa maoni, uhuru wa kuandamana na kutoa misimamo ni jambo ambalo linakubaliwa lakini pasipo kuharibu mali na balozi." Amesema Rais Mursi kupitia televisheni ya nchi yake huku pia akilaani mauaji ya balozi wa Marekani nchini Libya na kuahidi kulinda wageni.

Wizara ya afya ya Misri imesema watu kumi na tatu wamejeruhiwa katika maandamano hayo ambapo waandamanaji wameshusha bendera ya Marekani na kuichoma na kisha kupandisha bendera nyeusi.

Serikali ya Misri imetoa wito kwa raia wake kurejesha amani huku pia ikiikosoa filamu hiyo ambayo imeleta hasira nchini Libya na kusababisha vifo vya raia wanne wa Marekani akiwemo Balozi Chris Stevens mjini Benghazi.

Katika taarifa ya baraza la mawaziri iliosomwa na Waziri Mkuu Hisham Qandil , uongozi wa nchi hiyo umesema filamu hiyo imemdhalilisha Mtume Muhammad na pia imekiuka maadili. "Tunawaomba wananchi wote wa Misri kueleza hasira zao kwa amani," imeeleza sehemu ya tamko hilo.

Maandamano yasambaa katika ulimwengu wa Kiislamu

Ghasia katika maandamano ya kupinga filamu ya kumkashifu Mtume Muhammad mjini Cairo, Misri.

Ghasia katika maandamano ya kupinga filamu ya kumkashifu Mtume Muhammad mjini Cairo, Misri.

Maandamano ya kupinga filamu hiyo sasa yanaendeela kuenea katika nchi nyingine za Kiislamu, ikiwemo Morocco, Sudan na Tunisia.

Mjini Tunis polisi nao wamelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji.

Mjini Sanaa, Yemen, waandamanaji wenye hasira na filamu hiyo wamepambana vikali na polisi wakati wa maandamano yao nje ya ubalozi wa Marekani.

Filamu hiyo ambayo imesababisha machafuko na maandamano imeandaliwa na raia wa Marekani mwenye asili ya Kiyahudi ambaye anauelezea Uislamu kama kidonda ndugu na kumkashifu Mtume Muhammad .

Marekani yapeleka meli za kivita Libya

Wakati huo Marekani imetuma meli na manowari nchini Libya baada ya balozi wake kuuawa huku pia ikiamini kwamba shambulio hilo lilitekelezwa na al-Qaida na si raia wa kawaida.

Kiasi ya askari 50 wamepelekwa mjini Tripoli kwa ajili ya kuimarisha ulinzi katika ubalozi wake huku pia ikianza kuwaondoa wafanyakazi wake katika mji wa Benghazi.

Maandamano ya kulaani mauaji dhidi ya balozi wa Marekani nchini Libya.

Maandamano ya kulaani mauaji dhidi ya balozi wa Marekani nchini Libya.

Rais Barack Oboma wa Marekani ameitaka Libya kuimarisha ulinzi lakini pia akitaka hatua zaidi kuchukuliwa kwa wote waliohusika na mauaji hayo.

Katika taarifa yake hapo jana waziri wa mamabo ya nje wa Marekani Hillary Clinton alisema mashambulizi hayo yalifanywa na kundi dogo na si raia wala serikali ya Libya.

Maafisa wa Marekani wanachunguza tukio hilo lakini wakiamini kwamba huo ulikuwa mpango wa Al qaeda ambao wametumia maandamano kulipiza kisasi wakati wa kumbukumbu ya septemba 11.

Marekani imeendelea kuwaonya raia wake katika mataifa kadhaa kuepuka kukaa katika umati mkubwa lakini inaimarisha ulinzi katika balozi zake zote.

Na Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amelazimika kusitisha ziara yake nchini Norway akihofia ghasia zinazoweza kutokea kutokana na filamu hiyo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/ AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman