1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya virusi vya corona yazua hofu nchini Ujerumani

Tatu Karema
22 Oktoba 2020

Maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani yanazidi kuongezeka. Tafiti nazo zinazoonyesha kuzuka kwa hofu kutokana na ongezeko hilo la maambukizi pamoja na vizuizi vipya vya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

https://p.dw.com/p/3kHOf
Deutschland Iraks Ministerpräsident besucht Berlin
Picha: Stefanie Loos/AFP/dpa/picture-alliance

Leo Alhamisi Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani ya Robert Koch imerekodi maambukizi 11,287 katika muda wa saa 24 zilizopita. Idadi hiyo ni kubwa kabisa kutokea nchini Ujerumani kwani ni kwa mara ya kwanza maambukizi hayo kuzidi zaidi ya elfu 10 kwa siku.

Rekodi ya juu kabisa ya maambukizi ya mwisho iliwekwa Jumamosi ambapo maambukizi ya kila siku yalifikia 7,830. Huku maambukizi hayo yakizidi nchini Ujerumani utafiti uliofanywa na taasisi ya tabia ya watumiaji ya Growth from Knowlege au kwa kifupi GfK ya nchini Ujerumani, inaonyesha kwamba watumiaji wengi wanahofia janga la corona na maambukizi yanavyozidi kuongezeka Ujerumani.

Tafiti hiyo inaonyesha kwamba katika kipindi cha wiki mbili zilizopita robo tatu ya watu waliohojiwa wanahofia kwamba janga la corona linaleta kitisho kikubwa na ni nusu kati ya waliohojiwa wanahofia kuhusu hali zao za kiuchumi za baadaye. 

Merkel awataka raia wa Ujerumani kuwa makini

Akiwaasa Wajerumani katika kuzingatia vizingiti vilivyowekwa sasa kupunguza maambukizi ya corona katika kuhakikisha maambukizi hayaongezeki, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema kuwa sayansi inaonyesha kwamba maambukizi ya virusi vya corona yanahusiana na idadi ya watu tunaokutana nao kila siku na kwamba kama kila mtu atapunguza kukutana na watu nje ya familia yake katika kipindi cha sasa, mwelekeo huu wa maambukizi  huenda ukabadilika.

Janga hili la corona linaleta wasiwasi katika katika uchumi wa Ujerumani, kwani katika robo ya kwanza ulishaanguka. Tafiti hizi kuelekea watumiaji zinaleta wasiwasi kwamba uchumi utashuka zaidi kwani matumizi ya watu yatazidi kupungua kutokana na vidhibiti vilivyowekwa sasa vya kudhibiti janaga la virusi vya corona. Akizungumza na DW, mchumi Carsten Brzeski amesema kwamba mambo nchini Ujerumani yataendelea kuwa mabaya kutokana na ongezeko hilo la maambukizi pamoja na vizuizi vinayoendelea kuwekwa sasa kuzuia maambukizio hayo.