1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya corona yafikia milioni 4.7 ulimwenguni

Lilian Mtono
18 Mei 2020

Wakati visa vya maambukizi vikiongezeka kwa zaidi ya milioni 4.7 kote ulimwenguni, nchini Yemen watu 500 wamekufa katika kipindi cha siku nane zilizopita kusini mwa mji mkuu wa taifa hilo Aden.

https://p.dw.com/p/3cNEd
Guinea | Medizinisches Personal mit Schutzkleidung im Donka Krankenhaus in Conakry
Picha: Getty Images/AFP/C. Binani

Wengi wa wagonjwa walikuwa na tatizo la upumuaji, hali inayoibua wasiwasi kwamba virusi vya corona vinasambaa kwa kiasi cha kutoweza kudhibitiwa, kuzidi vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoliacha taifa hilo katika hali mbaya. 

Mchimbaji mmoja wa makaburi ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba hajawahi kuona idadi kubwa ya maiti katika mji ambao umeshuhudia mapigano makali wakati wa vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitano. Wengine wameripoti vifo zaidi ya kimoja, katika kipindi cha siku moja.

Watumishi wengi wa afya wanaokabiliwa na upungufu wa vifaa vya kujikinga wanaogopa kuambukizwa na vituo vingi vya afya mjini humo vimefungwa kwa kuwa watumishi wamekimbia na wengine wanawakataa wagonjwa. Maafisa na raia wanasema hata namba ya simu iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ya kuomba msaada wa huduma ya upimaji majumbani kwa wanaohiswa kuambukizwa haipokelewi.

Jemen | Corona Händehygiene in Slums
Binti akielekezana na mama yake namna ya kusafisha mikono katika kipindi hiki cha coronaPicha: UNICEF/UNI324948

Hata hivyo, afisa mmoja katika hospitali ya Al-Kubi, Mehdi al-Dabi amesema kwa siku wanapokea hadi wagonjwa 230 na wanawahudumia kwa usawa. Alisema "tunapokea zaidi ya wagonjwa 230 kwa siku, baadhi yao wanahisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona na wao tunawalaza pia. Tunawahudumia sawa wagonjwa wote tunaowapokea."

Soma Zaidi:Kipato duni kigezo cha kupata virusi vya corona 

Zaidi ya watu 314,000 wamekufa kote ulimwenguni kutokana na COVID-19 na zaidi ya milioni 4.7 wameambukizwa.

Nchini Ujerumani katika mji wa Cologne, watu 70 wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi wamegundulika kuambukizwa virusi vya corona. Watu 300 walifanyiwa vipimo na wale walioathirika walipelekwa kwenye makazi ya Mtakatifu Augustin, umbali wa saa moja kutoka Cologne.

Watu 60 ambao hawajaambukizwa walihamishiwa kwenye makaazi mengine.

Nchini Afrika Kusini kumeripotiwa visa vipya 1,160, idadi ya juu kabisa kuripotiwa kwa siku moja tangu mwezi Machi ambapo kulirekodiwa kisa cha kwanza. Wizara ya afya imesema, jimbo la Western Cape maarufu kwa utalii limerekodi takriban asilimia 60 ya idadi jumla ya visa nchini humo iliyofikia 15,515. Idadi ya vifo imeongezeka hadi 263.

Brasilien | Jair Bolsonaro
rais wa Brazil Jair Bolsonaro anakosolewa kwa kulipuuza janga la coronaPicha: Reuters/A. Machado

Huko Brazil, rais Jair Bolsonaro ameonyesha kupuuzilia mbali kanuni za kujitenga hapo jana, wakati taifa lake likikabiliwa na mripuko mbaya kabisa. Brazil imethibitisha idadi ya walioambukizwa ikipindukia ya Italia na Uhispania na taifa hilo sasa likiwa la nne kwa idadi kubwa ya maambukizi ulimwenguni. Wataalamu wanaonya huenda maambukizi yakawa ni zaidi ya 240,000.

Nchini Mexico, kumerekodiwa visa 49,219 hapo jana huku vifo vikifikia 5,177. Wataalamu wamesema taifa hilo limeshuhudia kuongezeka kidogo kwa maambukizi kuliko wastani wa kiulimwengu kutokana na maradhi yanayoongeza hatari ya kuambukizwa kama kisukari na uzito mkubwa.

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameziomba serikali kuajiri wauguzi wengi zaidi na kuwekeza kwenye mafunzo na mazingira ya kazi. Papa Francis amesifu kujitoa na ujasiri wa wauguzi akisema umuhimu wao umejidhihirisha kupitia janga hili la corona.

Mashirika: RTRE/AFPE/APE