1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUkraine

Ukraine yasema athari za kupasuka kwa bwawa zitaendelea

7 Juni 2023

Maafisa wa Ukraine wamesema uharibifu wa bwawa kubwa la maji la Kakhova uliotokea baada ya shambulizi la kombora utaendelea kuwa na athari za kutisha kwenye eneo la kusini mwa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/4SJUQ
Ukraine Kherson Überflutungen nach Dammbruch
Picha: Alina Smutko/REUTERS

Maafisa wa jeshi la nchi hiyo wamesema tangu kupasuka kwa kingo za bwawa hilo hapo jana, maji yameendelea kuvuja kwa wingi na kufurika kwenye vijiji vya eneo kubwa la kusini mwa Ukraine.

Hadi sasa maelfu ya watu tayari wamehamishwa kutoka jimbo la Kherson baada ya makaaazi kuzingirwa na maji. 

Andriy Pankratov ambaye ni mkuu wa kikosi cha uokoaj katika mji jirani wa Mykolaiv amesema, "Hapa Mykolaiv vikosi vya dharura vinatawanya mahema ya muda kuwapokea raia wanaotoka Kherson. Maji ya kunywa yanatolewa na uwezekano wa watu hao kuchaji simu zao."

Tathmini nyingine iliyotolewa kupitia taarifa ya kijasusi ya wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema kuta za bwawa hilo huenda zitadhoofika zaidi mnamo siku chache zinazokuja na kuongeza kiwango cha maji yanayovuja.