1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa saba wa polisi Mtwara wafikishwa mahakamani

Salma Mkalibala26 Januari 2022

Polisi saba mkoani Mtwara, Kusini mwa Tanzania wanatuhumiwa kufanya mauaji na kuutupa porini mwili wa mfanyabiashara wa madini aliyekuwa na umri wa miaka 25.

https://p.dw.com/p/465Oe
Tansania Grandpa Livembe
Picha: Salma Mkalibala/DW

Kijana Mussa Hamisi mkazi wa wilaya ya Nachingwea mkoa jirani wa Lindi, anadaiwa kukamatwa na askari wa polisi octoba 20, mwaka jana akiwa katika nyumba ya kulala wageni hapa Mkoani Mtwara akituhumiwa kuwa mwizi wa pikipiki na kufikishwa kituo cha poilisi kwa ajili ya mahojiano.

Baada ya kuhojiwa alibainika kuwa na fedha zipatazo shilingi million mbili na laki tano (2.5m), na kutaja kiasi kingine ambacho alikihifadhi nyumbani kwao wilayani Nachingwea Mkoani Lindi, ambako maofisa hao walifunga safari hadi wilayani humo katika nyumba ya wakazi wake kupekua na kubaini kiasi kingine cha dola za kimarekani 13,500 na kuondoka nazo wakiwa wamemuweka chini ya ulinzi.

Hawa Bakari ni mama mzazi wa kijana huyo, ambaye anasema mara ya mwisho kuonekana machoni mwa ndugu zake kijana wake ni januari 5, mwaka huu 2022, anaeleza namna askari walivyofika nyumbani kwao, kwa ajili ya kuchukua pesa alizokuwa nazo.

Soma pia: Bado hakuna mwafaka Mtwara

Kashfa mpya ya polisi Tanzania

Siku chache kijana huyo aliachiwa na jeshi la polisi kwa dhamana na kurudi uraiani bila kurejeshewa fedha zake, ndipo January 5 mwaka huu akiwa na mjomba wake anayeitwa Salum Ng,ombo walikwenda kituoni hapo kwa ajili ya  kufuatilia.

Soma pia : Polisi Tanzania yadai muuaji wa maafisa usalama alikuwa gaidi

Kufuatia tukio hilo, DW ilifika ofisi ya kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Mtwara ACP Marck Njera ili kujuwa ukweli, ambapo amethibitisha kufanyika kwa mauaji hayo na kubainisha kuwa jeshi hilo limewakamata na kuwafikisha mahakamani Maafisa wa Polisi saba kwa tuhuma hizo za mauaji lakini amesita kutaja njia ya mauji iliyotumika na maofisa hao.

Amesema tukio hilo lilifanyika January 5, mwaka huu na mwili wa marehemu ulitupwa katika pori la kijiji cha Hiari wilaya ya Mtwara.
Kando na maofisa hao saba, afisa mwingine ambaye anadaiwa kuhusika na mauaji hayo ni mkaguzi msaidi wa polisi Greyson Mahembe anatajwa kujinyonga kwa tambala la kudekia akiwa mahabusu ya polisi mkoani hapa.