1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa nchini Iran waondoa uwezekano wa kufuta matokeo.

Sekione Kitojo23 Juni 2009

Chombo kikuu kinachoangalia uchaguzi nchini Iran kimeondoa uwezekano wa kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais huku viongozi wa dunia wakieleza wasi wasi wao kuhusu hali nchini humo.

https://p.dw.com/p/IXKW
Picha hii inawaonyesha waungaji mkono kiongozi wa upinzani Mir Hossein Mousavi wakiandamana mjini Tehran.Picha: AP

Chombo kikuu kinachoangalia uchaguzi nchini Iran kimeondoa uwezekano wa kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais wakati dunia inaeleza wasi wasi wake katika ukandamizaji wa nguvu wa maandamano ya wapinzani wanaotoa changamoto kubwa kwa utawala wa Kiislamu nchini humo uliodumu sasa kwa muda wa miaka 30.

Msemaji wa baraza la wadhamini Abbasali Kadkhodai amenukuliwa akisema kuwa katika uchaguzi wa hivi karibuni wa rais tumeona hakuna udanganyifu ama ukiukaji wowote.

Upande wa upinzani umekuwa ukifanya maandamano karibu kila siku, wakidai kufanyika udanganyifu na mapungufu kadha katika uchaguzi wa hapo Juni 12 ambao umemrejesha rais mwenye msimamo mkali Mahmoud Ahmadinejad madarakani kwa muda wa miaka minne mingine.

Viongozi wa dunia wanatoa miito ya kusitishwa mara moja kwa matumizi ya nguvu yanayofanywa na serikali dhidi ya waandamanaji, huku vyombo vya habari vya taifa vikiripoti kuwa kiasi watu 17 wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa katika ghasia hizo ambazo zimelikumba taifa hilo kwa muda wa siku 11 sasa.

Mitaa ya mjini Tehran imeendelea kuwa na hali tete leo Jumanne siku ambayo maelfu ya polisi wa kuzuwia ghasia wakiwa na virungu vya chuma na wakifyatua mabomu ya kutoa machozi, wengi wakiwa katika pikipiki, walivunja maandamano ya wapinzani wapatao 1,000. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Robert Gibbs akiulizwa kuhusu rais hisia za rais Barack Obama kuhusu maandamano hayo alisema.

Ametiwa moyo na kile tulichokiona katika televisheni. Nadhani hasa ni kuhusu picha zinazoonyesha wanawake nchini Iran ambao wamejitokeza kutekeleza haki yao ya kuandamana, kutoa mawazo yao na kusikika.


Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameeleza wasi wasi wake mkubwa juu ya ghasia hizo na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa hatua za kuwakamata waandamanaji, vitisho na matumizi ya nguvu. Ameitaka serikali na wapinzani kutatua matatizo yao kwa njia ya amani na mazungumzo pamoja na njia za kisheria.

Baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza kuwataka raia wao kujiepusha kwenda Iran, nchi ambayo imekumbwa hivi sasa na mzozo mkubwa tangu mapinduzi ya Kiislamu miaka 30 iliyopita mzozo ambao unatishia msingi wa taifa hilo la Kiislamu.

Wakati huo huo chama cha wanafunzi wa Iran kimefuta maandamano yaliyopangwa kufanyika nje ya ubalozi wa Uingereza mjini Tehran leo Jumanne baada ya kupigwa marufuku na maafisa wa nchi hiyo.

Nae kiongozi wa upinzani nchini Iran Mir Houssein Mousavi amekutana na viongozi wa juu wa kidini na kujadiliana nao kuhusu hali ya mambo nchini humo, ikiwa ni pamoja na vifo vya waandamanaji wakati wa maandamano mitaani mjini Tehran.

Katika mkutano huo uliofanyika jana Mousavi amejadili kuhusu uchaguzi wa Juni 12, haki za raia kufuatilia suala hilo, ukamataji wa watu holela na mashambulizi dhidi ya waandamanaji ambayo yamesababisha vifo vya watu wasio na hatia.

Wakati huo huo duru katika wizara ya mambo ya kigeni nchini Iran zimekanusha kuwa balozi wa Uingereza nchini humo amerejeshwa nchini mwake kwa mashauriano.

Rais pamoja na baraza lake la mawaziri wataapishwa mbele ya jengo la bunge kati ya tarehe 26 Julai na August 19 kufuatia uchaguzi wa rais, limesema shirika la habari la Iran IRNA leo Jumanne.



Mwandishi:Sekione Kitojo/DPAE/AFPE

Mhariri: M.Abdul-Rahman

►◄