1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 yatangaza kusitisha mapigano

30 Agosti 2013

Kundi la waasi wa M23 katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo limesema kuwa linasimamisha mapigano mara moja, kuruhusu uchunguzi juu ya makombora yaliyovuka mpaka na kuanguka katika nchi jirani ya Rwanda.

https://p.dw.com/p/19Yyl
Waasi wa M23 mashariki mwa DRC
Waasi wa M23 mashariki mwa DRCPicha: Isaac KasamaniAFP/Getty Images

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lambert Mende, ameiambia DW mjini Kinshasa kuwa serikali ya nchi hiyo haijashangazwa na hatua hiyo ya M23, lakini akasisitiza kuwa wanachotaka wao ni kuona waasi hao wakiweka silaha chini, kama wanavyotakiwa na jumuiya ya kimataifa na pia serikali ya Kongo.

Jana, Rwanda ililishutumu jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kile ilichokiita uchokozi wa makusudi, baada ya kombora linaloaminika kutoka upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanguka nchini Rwanda, na kumuuwa mwanamke mmoja na kumjeruhi vibaya mtoto wake mchanga.

Serikali ya Kongo ilizikanusha mara moja tuhuma hizo, ikisema zilikuwa zikiashiria azma ya Rwanda kujiingiza waziwazi katika vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Kikomo cha uvumilivu

Kufuatia kifo cha mwanamke huyo katika mji wa Rubavu kaskazini magharibi mwa Rwanda, wizara ya mambo ya nje ya Rwanda ilitoa tangazo ambalo limesema nchi hiyo inao uwezo wa kujua yalikotoka mashambulizi dhidi yake, na kuonya kuwa haitasita kulinda eneo lake na kuwatetea wananchi wake.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda, Louise MushikiwaboPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, amesema katika kipindi cha mwezi mmoja, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limerusha mabomu yapatayo 34 ndani ya Rwanda. ''Tumejizuia tuwezavyo kuchukuwa hatua, lakini sasa hatuwezi kuendelea kuvumilia uchokozi huu.'' Amesema Bi Mushikiwabo.

Kongo yasema ni kisingizio

Akijibu tuhuma kutoka Rwanda kuwa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndilo linalorusha mabomu yanayoanguka nchini Rwanda, Waziri Mende amesema tuhuma hizo zinalenga kuhalalisha kujiingiza tena katika mikoa ya Kivu. ''Inachoazimia Rwanda ni kusababisha vurugu isiyokwisha ili iweze kuendelea kupora mali katika mikoa ya kivu, kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa miaka 15 iliyopita,'' alisema Mende.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa ulisema jana kwamba unazo ''ripoti za kuaminika'' za kuaminika, ambazo zinaonyesha kuwa wanajeshi wa Rwanda wameingia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Rwanda kuwasaidia waasi wa M23, katika vita linayopigana dhidi ya jeshi la Kongo na wanajeshi wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO.

Vita vya miaka mingi vimewahangaisha sana raia wa mikoa ya Kivu, mashariki mwa Kongo
Vita vya miaka mingi vimewahangaisha sana raia wa mikoa ya Kivu, mashariki mwa KongoPicha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Aidha, afisa wa ngazi ya juu wa MONUSCO, Ray Vilgilio Torres amesema vikosi vyao vimepata uhakika kuwa bomu lililomuuwa mwanamke nchini Rwanda, lilirushwa na waasi wa M23, kutoka ngome yao ya msitari wa mbele ya Kibati.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef