Müntefering ajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Müntefering ajiuzulu

Naibu kansela wa Ujerumani, Franz Munterfering, wa chama cha Social Democratic, SPD, amejiuzulu kwa sababu za kifamilia. Kujiuzulu kwake huenda kuzidishe hali ya wasiwasi katika serikali ya mseto inayoongozwa na kansela Angela Merkel mjini Berlin.

Müntefering na mke wake Ankepetra

Müntefering na mke wake Ankepetra

Naibu kansela wa Ujerumani, Franz Müntefering, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa chama cha SPD, anajiuzulu pia wadhifa wake wa waziri wa kazi. Kujiuzulu kwa kiongozi huyo ambaye mwaka wa 2005 alielezwa kuwa kiongozi aliyewanyanyasa wawekezaji wa kigeni, kutatoa mwanya kwa uwezekano wa kufanyika mabadiliko katika baraza la mawaziri la kansela Merkel.

Duru za chama cha SPD zinasema waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, ambaye katika kipindi cha miaka miwili iliyopita amechipuka kama kiongozi mwenye ushawishi mkubwa, huenda aichukue nafasi ya bwana Müntefering kama naibu kansela. Olaf Scolz, mbunge wa chama cha SPD, anatazamiwa kuteuliwa kuwa waziri wa kazi.

Franz Müntefering alikuwa kiongozi muhimu mwenye ushawishi mkubwa aliyeituliza misukosuko katika serikali ya mseto ya vyama vya SPD na muungao wa vyama vya kihafidhina, CDU-CSU. Kwa mantiki hiyo, kujiuzulu kwa Müntefering ni pigo kubwa kwa kansela Angela Merkel ambaye alishinda uchaguzi mkuu kwa idadi ndogo ya kura miaka miwili iliyopita. Bi Merkel ataukosa ushirikiano mzuri kati yake na bwana Müntefering.

Mwenyekiti wa chama cha CDU, Volker Kauder, amemueleza bwana Munterfering kama nguzo ya serikali. ´Franz Müntefering alikuwa nguzo ya serikali ya mseto. Franz Munterfering kila mara alifanya bidii kufikia ufanisi wa serikali. Amefanya kila aliloweza kuiwezesha serikali hii kufanikiwa. Tunamtakia kila la heri.´

Kuondoka kwa Müntefering serikalini pia kunatoa nafasi ya kutokea malumbano kutoka kwa chama cha SPD katika serikali ya kansela Merkel, huku uchaguzi muhimu wa mikoa ukikaribia mwaka ujao, na uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika mwaka wa 2009.

Mtaalamu wa siasa katika chuo kikuu cha hapa Bonn, Gerd Langguth, amesema Franz Müntefering ni kiongozi pekee aliyejitolea kwa dhati kuhakikisha serikali ya mseto inabakia na umoja.

Mke wa bwana Müntefering, Ankepetra, amekuwa mgonjwa sana akiugua ugonjwa wa saratani. Kuugua kwa mke wake kulimfanya Müntering asihudhurie mkutano muhimu wa serikali wiki iliyopita kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya. Msemaji wa wizara ya kazi mjini Berlin, Stefan Giffeler, amesisitiza kwamba waziri Franz Müntefering anajiuzulu kwa sababu za kifamilia na si vinginevyo.

Franz Müntefering, mwenye umri wa miaka 67, alikuwa mshirika wa karibu wa kansela wa zamani wa Ujerumani, Gerhard Schroeder, ambaye kutoka kwake alichukua hatamu za uongozi kama mwenyekiti wa chama cha SPD mwanzoni mwa mwaka wa 2004. Hata hivyo alijiuzulu wadhifa huo kabla miaka miwili kumalizika, wakati alipotofautiana na wanachama wengine wa chama hicho.

Müntefering alilumbana na mwenyekiti wa chama cha SPD bwana Kurt Beck mwezi uliopita ambapo Beck alimkososa hadharani Müntefering kwa kupendekeza kuondoa vipengele muhimu katika mpango wa mageuzi ya kiuchumi wa kansela wa zamani Gerhard Schroeder. Müntefering alishindwa katika malumbano hayo na Beck, hatua ambayo inahofiwa huenda imesababisha uamuzi wake kun´gatuka haraka.

 • Tarehe 13.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH6z
 • Tarehe 13.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH6z

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com