1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Luxembourg. Wapiga kura Luxembourg waidhinisha katiba ya Ulaya.

11 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CEvb

Wapiga kura nchini Luxembourg , wameidhinisha katiba ya umoja wa Ulaya katika kura ya maoni.

Nchi hiyo yenye wakaazi 465,000, ambayo ina ofisi kadha za taasisi za umoja wa Ulaya, jana Jumapili waliunga mkono katiba hiyo kwa wingi wa asilimia 56.52.

Matokeo hayo yatamruhusu waziri mkuu wa Luxembourg Jean Claude Juncker kuendelea na kazi yake kama alivyoahidi kujiuzulu iwapo nchi yake itaikataa katiba hiyo.

Mataifa yote 25 wanachama yanalazimika kuidhinisha katiba hiyo ama katika kura ya maoni ama katika kura ya bunge la nchi.

Katiba hiyo imekwisha idhinishwa na mataifa 13 ya umoja huo lakini imekataliwa na Ufaransa na Uholanzi katika kura ya maoni.

Kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder ameyakaribisha matokeo hayo ya kura ya maoni na kuyaeleza kuwa ni kitu ambacho wananchi wa Luxembourg wanaweza kujivunia. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Bwana Joschka Fischer amemsifu waziri mkuu Juncker kwa kufanya kampeni bila kuchoka na hatimaye kufaulu kwa kura ya ndio.