Luca toni atamba katika bundesliga | Michezo | DW | 18.02.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Luca toni atamba katika bundesliga

mshambulizi wa bayern Munich Luca Toni atia mabao 3 katika lango la hannover wakati Zamalek yaanza uzuri katika kombe la Afrika.

default

Munich na Hannover

Baada ya Holland na Ubelgiji jana kutoa maombi yao rasmi kwa FIFA kuandaa kombe la dunia 2018,rais wa FIFA Sepp Blatter, amedai mabara 2 –Afrika na Amerika kusini hayataruhusiwa kugombea mwaka huo kuandaa kombe la dunia.

Katika duru ya kwanza ya kombe la klabu bingwa barani Afrika mabingwa mara 5 wa Afrika-Zamalek ya Misri imeizaba APR FC ya Rwanda mabao 2-1 mjini Kigali na katika Ligi mashuhuri za ulaya, mshambulizi wa Itali-Luca Toni alitamba jana alipotia pekee mabao 3 katika lango la Hannover na kuifungulia klabu yake ya munich mwanya wa pointi 3 kileleni.

Jana, nchi mbili jirani Holland na Ubelgiji zilizoandaa kwa ubia kombe la Ulaya mwaka 2000 zilitoa maombi yao kwa pamoja kuandaa kombe la dunia 2018.Baadae, rais wa FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni-Sepp Blatter, alisema jana kwamba ingekuwa hawakuamua kuleta mfumo wa zamu ,bara la afrika linaloandaa kombe lijalo la dunia 2010 kamwe lisingepata nafasi ya kuandaa kombe la dunia.

Pia Amerika kusini ingeshindwa pia kuapata nafasi hiyo.Okotba mwaka jana ,halmashauri-tendaji ya FIFA ikabatiliosha mfumo huo wa zamu baada ya Afrika kusini kufaulu kuchaguliwa kuandaa kombe la dunia 2010 na Brazil, 2014.Blatter akasema Holland na Ubelgiji ndio za kwanza rasmi kutoa jana maombi yao kwa kombe la dunia 2018.

Mwenyeji atakaeandaa kombe la dunia 2018 ataamuliwa mwaka 2011-mwaka baada ya Afrika kusini kuandaa kombe la kwanza la Afrika.

Holland na Ubelgiji zatazamiwa kupewa changamoto na Mexico,Marekani,Uingereza,Ureno,Russia,china ,Japan na hata Australia.

Jana stadi maarufu wa dimba kabla enzi za Pele na Diego Maradona alitukuzwa-nae ni mzee wa asili ya argentina Alfredo Di Stefano alieichezea klabu bingwa mara kadhaa ya spain-Real Madrid.jana basi sanamu la stadi huyo di Stefano lilifunguliwa rasmi mjini Madrid.Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 81 sasa alitunukiwa jana tunzo maalumu kutoka kwa rais wa UEFA –shirikisho la dimba la ulaya Michel Platini aliemueleza mshambulizi huyo hatari kabisa zama zake „stadi mkubwa miongoni mwa mastadi wakubwa.“

Akasema,

„Katika dafutari la majina yalioandikwa kwa dhahabu katika historia ya dimba kuna ukurasa maalumu kwa Alfredo di Stefano.“ Alisema Platini.Di stefano alianza umaarfu wake alipoichezea klabu yake ya Argentina ya river Plate na akatia mabao mengi kwa klabu ya Millonarios,ndie aliekuja kuipa jina barani ulaya Real madrid ya Spain alipoiongoza kutwaa mfululizo vikombe vya klabu bingwa barani ulaya kati ya 1956 na 1960. Akiwa amechaguliwa mara 2 mchezaji bora wa dimba barani ulaya 1957 na 1959,Di Stefano alitia jumla ya mabao 418 katika mechi 510 kwa Real madrid na katika maisha yake ya kabumbu ya miaka 20,alitia jumla ya mabao 900.

Katika Bundesliga,mshambulizi wa timu ya taifa ya Itali,Luca Toni jana alilifumania mara 3 lango la Hannover na kuipatia ushindi uliobakisha mwanya wa pointi 3 kileleni kati ya Munich na Werder Bremen.

Mnamo dakika ya 58 ya mchezo Luca Toni alivunja tumbuu ya lango la hannover,halafu utamua ulipomkolea wa kutia mabao alirudi tena na halafu tena kuizamisha hannover kwa mabao yake 3.Ushindi huo uliipatia Munich jjumla ya pointi 43 kileleni mwa Ligi kwa 40 za Bremen.

Akitoa pongezk nyingi kwa stadi wake Luca Toni,kocha wa Bayern Munich, Ottmar Hitzfeld alisema:

„Anahitaji nafasi chache tu kugeuza mabao.Ana uchu wa mabao na karibu na lango la adui ana ufundi ajabu wa kufunga magoli.Akiwa mtiaji magoli mengi tayari huko kwao Itali,hakuna haja hapa kuzungumza mengi juu ya sifa zake.“-alisema kocha wa Bayern Munich Ottmar hitzfeld.

Hamburg jana iliparamia ngazi hadi nafasi ya 3 nyuma ya Munich na Bremen kwa kuikomea Bochum mabao 3-0.

KOMBE LA KLABU BINGWA AFRIKA:

Duru ya kwanza ya kombe la klabu bingwa barani Afrika ilianza mwishoni mwa wiki huku mabingwa mara 5 wa kombe hilo Zamalek ya Misri,wakiania kufuata nyayo za timu yao ya Taifa-Misri iliotoroka majuzi huko Ghana na kombe la Afrika la mataifa kwa mara ya 6 .

Zamalek nayo ina nia ya kulitwaa msimu huu kwa mara ya sita na ilianza uzuri mjini Kigali hapo jumamosi ilipoitimua APR FC ya Rwanda kwa mabao 2:1.Alikua Moustafa Gaafar alielifumania lango la APR kwanza katika kipindi cha kwanza kabla mwenzake Gamal Hamza kupachika bao la pili mnamo dakika ya 71 ya mchezo.

Mabingwa wa zamani kama zamalek Hearts of Oak kutoka Ghana walikiona kilichomtoa kanya manyoya mbele ya FC 105 ya Gabon.Union Douala ya Kamerun walizabwa nao mabao 3-1 na ASKO Kara ya togo. Club Africain ya tunisia walitamba kwa mabao 2-1 mbele ya ACS Saloum ya Senegal. Motema Pembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya kongo imeitandika Goma Utd ya Nigeria mabao 2:0 nayo Starlight ya Mauritious imeionea Mitsamiouli ya Comoro kwa mabao 2:0.

Mjini Dar-es-salaam, samba walinguruma mbele ya Awassa City ya Ethiopia katika kombe la CAF huku Miembeni ya Zanzibar ikizabwa bao 1:0 nyumbani na mamelodi sundowns ya Afrika kusini.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com