1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LSK kuwasilisha ombi la kumshitaki Rais Uhuru Kenyatta

Shisia Wasilwa
9 Juni 2020

Chama cha Wanasheria kimesema kitawasalisha ombi kwenye bunge la taifa kwa lengo la kuanzisha mchakato wa kumshitaki rais Uhuru Kenyatta.

https://p.dw.com/p/3dWfQ
Kenia Symbolbild Wahlen und Social Media
Picha: AFP/T. Karumba

Rais wa Chama cha Wanasheria LSK Nelson Havi anadai kuwa Rais Kenyatta amekwenda kinyume na katiba

Kauli hiyo ya Rais wa Chama Cha Wanasheria inajiri muda mfupi baada ya Rais wa Idara ya Mahakama Jaji David Maraga kumkosoa rais Kenyata kwa kukataa kukutana naye ili kujadili kuteuliwa kwa majaji 41 kama ilivyopendekezwa na Tume ya Kuajiri Maafisa wa Idara hiyo.

Nelson Havi amesema kuwa miezi sita inakamilika tangu Jaji Mkuu, Maraga kutoa ombi la kuwalisha kiapo majaji hao, lakini rais Kenyatta amepuuza.

Havi amesema hatua hiyo imeathiri utendakazi wa mahakama kiasi kuwa, kesi zinazidi kurundikana, huku majaji wa kuamua wakiwa wachache. Rais wa chama hicho amesema: "Tunatoa ombi kwa bunge la Taifa na Seneti, kuanza mchakato wa kumfungulia mashtaka Rais wa Jamhuri ya Kenya, kwa sababu, hatuwezi tukawa na mtu aliyekula kiapo cha kutii katiba, anashindwa kutekeleza majukumu yake.”

Havi amesema kuwa rais alikula kiapo cha kuzingatia na kudumisha katiba, jinsi maafisa wengine wa umma walivyofanya akiwemo rais wa Idara ya Mahakama, David Maraga. Chama cha Wanasheria kimeanza mchakato wa kuwaondoa Mwanasheria Mkuu Paul Kihara na Wakili Mkuu katika afisi ya Mwanasheria Mkuu Kennedy Ogeto kutoka kwenye orodha ya mawakili.

Wanadai kuwa wameshindwa kumshauri rais kuhusu masuala ya katiba. Iwapo kitafanikisha malengo yake, Kihara na Ogeto hawatakuwa mawakili katika mahakama Kuu. Tayari chama hicho kimewatumia nyaraka kikitaka wajieleze, huku kikiwapa siku saba kufanya hivyo.

David Maraga amkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kuupuza sheria

Kenia Supreme Court Richter David Maraga
Rais wa Idara ya Mahakama David MaragaPicha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Ni bayana kuwa Idara ya Mahakama inakwaruzana na mhimili wa utawala wa Urais.

Akihutubia wanahabari hapo jana, Rais wa Idara ya Mahakama David Maraga, bila ya maafisa wengine katika idara hiyo, alimkosoa rais Kenyatta na serikali yake, kwamba inaonekana kupuuza sheria. Maraga amesema kuwa serikali imeshindwa kutekeleza maamuzi mengi yaliyotolewa na mahakama mbali mbali dhidi yake. 

Mapema mwaka huu Maraga na Rais Kenyatta walikutana hivyo kuonekana kutatua mzozo kati ya mihimili hiyo ya utawala, hata hivyo matamshi ya Jaji Maraga Jumatatu yanadhihirisha bayana kuwa, mikwaruzo kati yao haijapigwa msasa.

Maraga amesalia na miezi sita kuondoka kwenye kiti hicho.

Hata hivyo Chama cha Wanasheria nchini, kina kibarua kizito na kigumu, ikizingatiwa kuwa rais Kenyatta ana idadi kubwa ya wabunge kwenye Bunge la taifa na Baraza la Seneti wanaomuunga mkono.

Aidha Chama cha Upinzani kinachoongozwa na Raila Odinga yaelekea kuwa kimemezwa na serikali hivyo kushindwa kumkosoa rais.