1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Polisi wawahoji washukiwa

2 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBme

Polisi nchini Uingereza leo wanaendelea kuwahoji washukiwa watatu wa njama ya ugaidi waliojaribu kulipua mabomu mawili yaliyokuwa yametegwa ndani ya motokaa mbili katikati mwa mji wa London.

Juhudi zimeanza pia za kuwatafuta washirika wa watu wanaotuhumiwa kuwa wanamgambo waliojaribu kuingiza gari iliyokuwa ikiwaka moto ndani ya uwanja wa ndege wa Glasgow nchini Scotland.

Duru za polisi zinasema msako umeanza kuwatafuta watu kadhaa kufuatia kukamatwa kwa washukiwa watano wa njama hiyo ya kigaidi.

Kamanda wa kitengo cha polisi kinachopambana na ugaidi Peter Clarke amesema uchunguzi unaoendelea unafichua mambo mengi kuhusu watu waliohusika kwenye shambulio kjatika uwanja wa ndege wa mjini Glasgow na yale yaliyopangwa kufanywa mjini London.

Clarke amesema uhusiano kati ya mashambulio matatu unazidi kuwa wazi na wanafuatilia njia mbalimbali za uchunguzi. Ana hakika katika siku chache zijazo wataweza kufahamu kikamilifu mbinu zinazotumiwa na magaidi, jinsi wanavyopanga mashambulio yao na mtandao wao.

Waziri mkuu wa Uingereza bwana Gordon Brown, akikabiliwa na mtihani mkubwa katika siku zake za mwanzo kwenye wadhifa huo, amesema waliopanga njama hizo za kigaidi wana mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Wakati huo huo, rais George W Bush wa Marekani amempongeza bwana Gordon Brown kwa jinsi alivyoishughulikia njama ya kuyashambulia maeneo mawili ya mjini London na shambulio kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Glasgow.