1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Blair awatolea mwito wanasiasa wa Ireland Kaskazini

9 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKo

Waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair, na mwenzake wa Ireland Kaskazini, Bertie Ahern, wamewatolea mwito wanasiasa wa Ireland Kaskazini watumie nafasi hii kuzifufua shughuli za bunge litakalogawana madaraka nchini humo.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza kandoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji. Tony Blair amesema wanasiasa waliochaguliwa nchini Ireland Kaskazini wana jukumu la kuwasilikiliza wananchi.

´Watakachotaka kukifanya wanasiasa waliochaguliwa nchini Ireland Kakszini ni kuwasilikiliza wananchi. Nafikiri wananchi kwa njia fulani wameonyesha uongozi katika uchaguzi huu kwa sababu walichosema juu ya kugawana madaraka kinatakiwa kutimizwa. Nafikiri raia wanawaambia wanasiasa tunataka muyashughulikie maswala yanayotuhusu.´

Chama kikubwa cha kiprotestanti, Democrtic Unionist Party, DUP, kimekishinda chama cha kikatoliki cha Sinn Fein katika uchaguzi wa bunge. Vyama hivyo vitakiwa viunde serikali mpya itakayogawana madaraka nchini humo.

Kwa mujibu wa mkataba wa amani uliotayarishwa na Uingereza na Ireland, vyama vimepewa hadi tarehe 26 mwezi huu kuunda serikali mpya.

Ireland Kaskazini imekuwa ikitawaliwa kutoka mjini London tangu mwezi Oktoba mwaka wa 2002, wakati madai ya ukachero uliofanywa na bawa la kijeshi la chama cha Sinn Fein, IRA, uliposababisha bunge kusitisha shughuli zake. Matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa baadaye leo.