Liverpool yachukua usukani wa ligi ya England | Michezo | DW | 07.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Liverpool yachukua usukani wa ligi ya England

Liverpool walipanda kileleni mwa Premier League kwa kishindo baada ya kuonyesha kwa mara nyingine uwezo wao wa ushambuliaji chini ya ukufunzi wa Jurgen Klopp kwa kuiangamiza Watford 6-1

Baada ya Arsenal kukosa fursa ya kuruka mbele ya viongozi wa muda Chelsea baada ya kutoka sare ya 1-1 na mahasimu wao wa London Tottenham Hotspur, Liverpool waliitumia ipasavyo nafasi hiyo kwa kuwazidi nguvu wageni Watford.

Chelsea ambayo inashikilia nafasi ya pili kwenye ligi, pia ilipata ushindi mnono wa 5-0 dhidi ya Everton siku ya Jumamosi na kudhihirisha uwezo wa timu inayotafuta ubingwa hasa ikizingatiwa kuwa haina kandanda la Ulaya msimu huu kama tu ilivyo Liverpool.

Ushindi wa Manchester United katika mechi tano za ligi wa 3-1 dhidi ya Swansea ulikuwa kitulizo kwa kocha Jose Mourinho baada ya wiki yenye majaribu. Lakini licha ya ushindi huo, Mourinho alionekana kuwakashifu wachezaji wake ambao anahofia kuwa huenda wasiwe na mtazamo sahihi kuirejesha timu yake katika kinyang'anyiro cha ubingwa wa ligi. Mourinho alizungumzia wazi haja ya wachezaji kucheza kwa kujituma licha ya wao kuwa na maumivu au majeruhi. Anasema wachezaji wanapaswa kucheza hata kama hawako tayari kwa asilimia 100.

La liga

Nchini Uhispania Barcelona ilitoka nyuma na kuishinda Sevilla mabao mawili kwa moja jana kupitia mabao ya Lionel Messi na Luis Suarez na kubakia nyuma ya Real Madrid na pengo la pointi mbili tu. Real Madrid iliwachabanga Leganes 3-0 na kuchukua usukani wa ligi. Baada ya mechi 11, Real wana pointi 27, Barcelona wana 25 na Villarreal wana 22. Kisha Atletico Madrid na Sevilla zote katika nafasi ya nne, pointi 21 kila mmoja.

Mwandishi:_Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu