1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liverpool waonyesha uwezo wao kwa kuwabwaga Spurs

Bruce Amani
28 Oktoba 2019

Liverpool wameonyesha kwa mara nyingine jana kuwa wana uwezo wa kupambana na kupaza matokeo muhimu hata wakati mambo yanaonekana kuwa magumu uwanjani. Hii ni baada ya kutoka nyuma na kuishinda Spurs 2 – 1.

https://p.dw.com/p/3S4oc
Fußball Champions League - Gruppe E - KRC Genk v Liverpool
Picha: Reuters/P. Childs

Kocha wa Liverpool aliwapongeza vijana wake kwa namna walivyojiamini na kupata pointi tatu zilizorejesha pengo lao la pointi sita kileleni mwa Premier League. Spurs wameshuka kabisa kwenye ligi wakiwa na pengo la pointi 16 nyuma ya Liverpool.

Ole Gunnar Solskjaer amejihisi ahueni baada ya Manchester United kupata ushindi wao wa kwanza wa ugenini katika miezi minane kwenye premier league wakati timu yake iliishinda Norwich City 3 – 1. Ushindi huo umewaweka Utd katika nafasi ya saba kutoka ya 14.

Nahodha wa Arsenal Granit Xhaka alionekana akitumia lugha ya matusi dhidi ya mashabiki wa timu yake baada ya kuondolewa uwanjani katika kipindi cha pili wakati Crystal Palace walitoka nyuma 2 – 0 na kutoka sare ya 2 – 2. Uamuzi wa kocha Unai Emery kumuondoa Xhaka kwanza ulipokelezwa kwa shangwe na mashabiki, na muda mfupi baadaye wakaanza kumzomea alipojikokota kuondoka uwanjani. Emery amesema watalitatua suala hilo. Arsenal walinyimwa bao la tatu kupitia uamuzi wa VAR.

Na tukibaki huko huko England ni kuwa wachezaji na benchi la kiufundi la Southampton wamekubaliana kutoa mshahara wao wa Ijumaa iliyopita kwa Shirika la Hisani la Saints katika hatua ya kwanza ya kujikomboa kufuatia kichapo cha 9 – 0 dhidi ya Leicester City. Taarifa ya klabu hiyo imesema kuwa kikosi chao kimekuwa mazoezini wikendi nzima kikiyaweka mambo sawa kwa ajili ya mashabiki klabu hiyo.