Liu Xia awekwa katika kizuizi cha nyumbani. | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Liu Xia awekwa katika kizuizi cha nyumbani.

Mke wa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu, Liu Xiaobo, Liu Xia amewekwa katika kizuizi cha nyumbani mjini Beijing, muda mfupi tu baada ya kumtembelea mumewe gerezani, kumfahamisha juu ya tuzo aliyoshinda.

default

Mke wa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2010, Liu Xia, ambaye amewekwa katika kizuizi cha nyumbani.

Kwa kutumia mtandao wa Twitter, Bibi Liu Xia alifahamisha juu ya kizuizi cha nyumbani alichowekewe mwishoni mwa wiki iliyopita, muda mfupi baada ya kumtembelea mume wake na kwamba anasema hafahamu ni lini ataweza kumuona mtu yoyote na kuomba msaada kwa masahibu hayo yaliyomkumba.

Anasema alikutana na mume wake gerezani alipokwenda kumtembelea Jumamosi ya wiki iliyoisha.

Mashirika mawili ya haki za binadamu ya Marekani likiwemo moja lenye makao yake nchini China -HRIC- yamethibitisha kuzuiliwa kwa mama huyo.

Katika taarifa yake, Shirika hilo la -HRIC- limeitaka jumuia ya kimataifa kwa nguvu zote kuzishinikiza mamlaka nchini China kumuachia haraka Liu Xia kutoka katika kizuizi hicho cha nyumbani na kuwaachia huru wafungwa wengine wote waliofungwa kutokana na kuelezea haki yao ya uhuru wa kujieleza.

China / Liu Xia / Hausarrest / Peking

Waandishi wa habari wakijaribu kuingia nyumbani kwa bibi Liu Xia mjini Beijing:

Aidha wanaharakati hao pia wamesema kwamba , baada ya kumtembelea mumewe gerezani, mama huyo alinyang'anywa simu na hivyo kumfanya kukosa mawasiliano.

Wakati huohuo Liu Xiaobo raia wa kwanza wa China kushinda tuzo ya Nobel ya amani ameitoa tuzo yake hiyo kwa wale wote waliouawa katika tukio la ukandamizaji wa watu waliokuwa wakidai demokrasia katika uwanja wa Tiananmen, lililotokea mwaka 1989, ambapo serikali ya China ilipambana na wanafunzi walioandamana.

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la HRIC lilimnukuu mku wa Liu Xiaobo akisema kwamba mume wake alitokwa na machozi baada ya kutoa maneno ya kuwaenzi wamnaharakati hao waliouawa, ambao wengi wao walikuwa ni wanafunzi.

Maafisa nchini China wamewatia kizuizini wafuasi wa mshindi huyo katika miji ya Beijing, Shanghai na miji mingine nchini humo, wakati walipokuwa wakisherehekea tuzo yake hiyo aliyoipata.

Jana polisi waliweka vizuizi katika barabara za kuelekea kwenye gereza alilofungwa mwanaharakati huyo, huku watu wachache ndio waliokuwa wakiruhusiwa kuingia katika eneo hilo la gereza na kwamba simu katika gereza hilo zilikuwa hazijijibiwi.

Liu Xiaobo alishinda tuzo ya amani ya Nobel siku ya Ijumaa kutokana na miongo miwili ya harakati zake zisizotumia nguvu ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaheshimiwa nchini China.

Liu ni mmoja ya watu watatu ambao walizawadiwa tuzo hiyo wakati wakiwa gerezani, baada ya kuhukumiwa na serikali za nchi zao. Mwingine ni kiongozi wa upinzani wa Myanmar Aung Sang Suu Kyi.

Mwandishi: Halima Nyanza (afp)

Mhariri: Sekione Kitojo.

 • Tarehe 11.10.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Paxq
 • Tarehe 11.10.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Paxq
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com