1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Licha ya Majanga mbalimbali yaliyoikumba Msumbiji, Uchumi wake unaonekana kuendelea kukua.

Scholastica Mazula25 Aprili 2008

Malengo ya Msumbiji ya kukuza uchumi wake kwa asilimia nane mwaka huu yanaweza kutekelezwa, licha ya nchi hiyo kukumbwa na Mafuriko na Vimbunga ambavyo vimekuwepo katika kipindi cha mwaka huu.

https://p.dw.com/p/Dojn
Rais wa Msumbiji Armando Emilio Guebuza.Picha: picture-alliance/dpa

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki Kuu nchini Msumbiji.

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Msumbiji, Michael Baxter, amesema kutokana na ongezeko la kukua kwa uchumi ambao mwaka 2007 ulifikia asilimia nane nukta nne, hali hiyo inaweza kuendelezwa hata katika kipindi cha mwaka huu.

Katika mahojiano yake na shirika la habari la Reuters mwanzoni mwa wiki hii, Bwana Baxter, alisema kuwa wanaamini na kila mtu anakubaliana nao kwamba kukua kwa uchumi kufikia asilimia nane ni jambo linalowezekana licha ya majanga yote yaliyoikumba nchi hiyo.

Benki ya Dunia ni mfadhili mkubwa nchini Msumbiji ambako Uchumi wake mwaka 2007 ulikuwa asilimia saba nukta tano na misaada ya Benki imetoa kipaumbele kusaidia bajeti na miradi ya ujenzi mpya nchini humo.

Serikali imechangamka kuendeleza miundombinu na mitambo ya nishati kwa sababu ya Makampuni ya kigeni kuvutiwa na utajili wa maliasili na madini ya nchi hiyo, hali itakayoweza kuimarisha biashara katika kanda hiyo.

Misaada ya kigeni imekuwa ikichangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa Kiuchumi nchini humo lakini biashara ndogondogo na za kati zinakuwa polepole kwa sababu ni vigumu kwa biashara hizo kupata misaada ya kifedha.

Msumbiji ilikuwa ni moja kati ya nchi masikini duniani baada ya kumalizika kwa miaka kumi na saba ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992, lakini pia imekuwa ni moja ya nchi iliyoko Kusini mwa Afrika ambayo Uchumi wake umekuwa ukikua kwa zaidi ya miongo kadhaa iliyopita.

Serikali ya Koloni hilo la zamani la Ureno, imeanzisha mageuzi ya kuimalisha uchumi.

Hata hivyo misaada ya wafadhili na utulivu wa kisiasa nchini humo umesaidia kuimarisha uchumi.

Lakini mbali na nchi hiyo kuwa na mikakati mbalimbali ya kukuza uchumi wake, idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo wapatao milioni ishirini huishi katika hali ya umasikini na kilimo cha kujipatia mahitaji yao ya kawaida.

Mkurugenzi wa Benki ya dunia nchini humo bwana Baxter anasema uwekezaji ndiyo utakaoweza kukuza zaidi uchumi wa nchi hiyo pamoja na kwamba changamoto zilizopo nikuongeza ukuaji na kuweza kumudu bajeti.

Baxter ambaye pia ni msimamizi wa shughuli za Benki Kuu katika nchi za Angola, Malawi.Zambia na Zimbabwe, anasema kwamba suala la kuongeza ukuaji wa Kiuchumi nchini Msumbiji linawezekana kwa sababu miradi mbalimbali mikubwa imekuwa ikiendelea kukua huku uwekezaji ukiwa unaongeza talii.

Mbali na kwamba Msumbiji ina hamu kubwa ya kupata wawekezaji wa kigeni, lakini bado kuna haja ya nchi hiyo kulifanyia ukarabati bwawa la umeme la Cabora Bassa ambalo lilijengwa na wakoloni wa Kireno mwaka 1960 na baadaye likatelekezwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya Uhuru wa nchi hiyo mwaka 1975.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali mjini Maputo, Bwawa la Cabora Bassa limekuwa likizalisha umeme wenye nguvu za Megawati elfu kumi na nne ikiwa ni mara saba ya kiwango cha uzalishaji cha sasa.Lakini kuweza kufikia kiwango hicho kunahitaji uwekezaji mkubwa zaidi.

Mwaka jana China ilikuwa ni nchi ya sita kwa uwekezaji nchini Msumbiji wakati marekani ikiongoza kwa uwekezaji kufikia dola bilioni tano.

Kituo cha uwekezaji cha msumbiji -CPI, kimesema China imeweza kuwekeza kwa dola milioni sita katika miradi kumi na moja ambayo iko kwenye kilimo, misitu, maji na kazi mbalimbali za kijamii.