Licha ya maafa ya Japan, bado Afrika yataka nyuklia | Matukio ya Afrika | DW | 22.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Licha ya maafa ya Japan, bado Afrika yataka nyuklia

Wakati barani Ulaya ukiendelea mjadala mzito baada ya janga la mionzi ya nyuklia ya Japan, baadhi ya mataifa ya Afrika yangali yanaona kuwa nishati ya nyuklia ndilo suluhisho la tatizo la umeme linalowakabili.

Moshi katika kinu cha nyuklia cha Fukushima Daiichi

Moshi katika kinu cha nyuklia cha Fukushima Daiichi

Linapokuja suala la nyuklia na nishati ya atomiki duniani, bado Afrika ni safi, ukiacha kile kinu cha Körbel, katika pwani ya magharibi ya Afrika ya Kusini.

Lakini kuna mataifa barani humo, ambayo yangelipenda kubadilisha sura hii. Nigeria, kwa mfano, inapanga kuwa ndani ya kipindi cha miaka 10 hadi 15 ijayo, inatumia nishati hiyo. Na kwa mujibu wa mkuu wa Kamisheni ya Nishati ya nchi hiyo, Sani Sambo, kilichotokea Japan hakijaibadilisha dhamira yao.

"Jambo hilo halina madhara yoyote kwetu. Bado tunabakia kuwa taifa ambalo lina matarajio ya kuwa na nishati ya nyuklia hapo baadaye." Anasema Sambo.

Suala la usalama wa vinu vya kiatomiki, kwa nchi kama hii ambayo asilimia 40 ndiyo inayopata huduma ya umeme, halijadiliwi kabisa. Sambo anaona kuwa, jambo kama hilo ni mjadala kwa nchi magharibi, ambazo zina njia nyengine za kupata nishati bila kutumia nyuklia, na sio kwa Nigeria.

Nyuklia

Nyuklia

Nchi nyengine za Afrika, kama vile Senegal, Namibia, Uganda na Kenya, nazo zimekuwa zikifikiria kuwa na nishati ya atomiki na kuomba uchunguzi wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Kimataifa, IAEO. Kwa miaka mingi sasa, Shirika hili limekuwa likishinikiza ujenzi wa vinu vya nyuklia katika bara hilo.

Na hadi sasa haifahamiki kuwa kile kilichotokea Japan kimeweza kubadilisha mawazo ya shirika hili, maana wenyewe hawako tayari kuzungumzia hilo.

Hata hivyo, kwenye mtadao wake, mtu anakutana na picha ya video ya mkuu wa kitengo cha Afrika, Ali Boussaha, akipigia debe nishati ya atomiki kwa Afrika, kwamba ndiyo inayohitajika kwa sasa katika bara hilo.

Vile vile, mataifa mengine ya Ulaya yanawashajiisha maraisi wa Kiafrika kujiingiza kwenye mpango huu wa nishati ya nyuklia. Takribani miaka minne iliyopita, Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkuzy, alikubaliana na Kanali Muammar Gaddafi wa Libya kufanya kazi pamoja kwenye mradi wa ujenzi wa kinu cha nyuklia katika nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini.

Hata hivyo, baadaye Kanali Gaddafi aliachana na mpango huo, lakini hivi karibuni Rais Sarkuzy alikutana na Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, kuzungumzia biashara ya nyuklia baina ya nchi zao.

Kwa watetezi wa mazingira duniani, Afrika ni sehemu mbaya zaidi kwa atomiki, maana haina uzoefu wa kutosha wala miundo mbinu madhubuti ya kuweza kumudu teknolojia hii. Wanasema kuwa, laiti yaliyotokea Japan yangeliipata Afrika yenye vinu vya nyuklia, matokeo yangelikuwa mabaya zaidi.

"Wanatakiwa waone hali halisi ilivyo. Ikiwa Japan, nchi yenye utaratibu mzuri na viwango vya juu vya usalama, haikuweza kulizuwia janga hili, bila ya shaka, kwa Afrika ingelikuwa hasara kubwa sana kama yangelitokea haya huko." Anasema Rianne Teule, mtaalamu wa nyuklia katika Shirika la Kimataifa la Utetezi wa Mazingira, Greenpeace, kanda ya Afrika.

Hata hivyo, bado kuna wataalamu wengine, kama vile mtafiti wa nyuklia wa Ethiopia, Gedion Getahun, ambao wanaona kuwa, pamoja na matukio ya Japan, bado uwezekano wa Afrika kuwa na nishati ya nyuklia ni kitu kinachowezekana.

Kwa sababu wakati nchi za viwanda, kama vile Ujerumani, zitakapofunga vinu vyake, makampuni ya nyuklia yatatafuta masoko mapya. Na itakayokuwa juu kwenye orodha yao itakuwa Afrika, ambayo hadi sasa ingali ardhi isiyo na mwenyewe katika suala la atomiki.

Mwandishi: Jan-Phillip Scholz/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza