Hakimi ajumuishwa kikosi cha PSG dhidi ya Monaco
25 Februari 2026
Wakili wa Hakimi pamoja na mwendesha mashtaka wa Ufaransa walitangaza siku ya Jumanne, kwamba beki huyo wa PSG na timu ya taifa ya Morocco atashtakiwa mahakamani kwa kosa la kumbaka mwanamke kijana.
Mnamo Februari 2023, mwanamke mwenye umri wa miaka 24 wakati huo aliieleza polisi katika eneo la Val-De-Marne, kusini mashariki mwa Paris, kwamba Hakimi alimrubuni na kumbaka.
"Leo, shtaka la ubakaji linatosha kuhalalisha kesi kufunguliwa mahakamani, ingawa nalipinga na kila ushahidi unaonyesha kwamba ni la uongo," aliandika Hakimi kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumanne.
"Ninasubiri kesi hii kwa utulivu, kwani itaruhusu ukweli kuwekwa wazi hadharani."
Wakili wa Hakimi, Fanny Colin, alihoji ushirikiano wa mwanamke huyo katika uchunguzi. "Mahakama imeamuru kesi kufunguliwa kwa msingi wa shtaka linalotegemea tu kauli ya mwanamke ambaye alizuia uchunguzi wote, alikataa kufanyiwa vipimo vyote vya kitabibu na DNA, alikataa kukaguliwa simu yake ya mkononi, na alikataa kutoa jina la shahidi muhimu," alisema Colin.
Wakili wa mlalamikaji, Rachel-Flore Pardo, alisema mteja wake amepata faraja baada ya kusikia kesi hiyo itaendelea mahakamani. Aliongeza kuwa vyombo vya sheria vimekuwa mfano bora katika kushughulikia suala hilo.
Hakimi alihudhuria mazoezi ya kabla ya mechi ya PSG siku ya Jumanne, na kwa kawaida angekuwa chaguo la moja kwa moja katika nafasi ya beki wa kulia kwa mabingwa wa Ulaya watakapowakaribisha Monaco kwenye Uwanja wa Parc des Princes wakiwa mbele kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya mchezo wa kwanza wiki iliyopita.
Kocha wa PSG, Luis Enrique, alipohojiwa kuhusu kesi ya Hakimi katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa, alisema, "Jambo hili liko mikononi mwa mamlaka husika.”