Libya yaanza kujijenga upya | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.09.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Libya yaanza kujijenga upya

Viongozi wa Libya wameahidi kuchunguza madai ya "uhalifu wa hali ya juu" baada ya benki kuu ya dunia kuwatambua kama wawakilishi rasmi wa serikali ya Libya.

default

Kiongozi wa Baraza la Mpito la Taifa la Libya, Mustafa Abdel Jalil

Baraza la mpito la taifa lilikuwa likijibu ripoti iliyochapishwa jana na shirika linalopigania haki za binaadam - Amnesty International, inayowatuhumu wanamgambo waliouangusha utawala wa Muammar Gaddafi.

Baraza la mpito la taifa linasema limearifiwa kuhusu baadhi ya visa vinavyowahusu wale wanaompinga Gaddafi na limedhamiria kuchunguza madai ya Amnesty International.

Shirika hilo linalopigania haki za binaadam limesema mnamo siku za mwanzo za machafuko,wapinzani wa Gaddafi waliwauwa wanajeshi kadhaa waliokamatwa pamoja na watu waliokuwa wakituhumiwa kuwa mamluki.

"Baadhi wamepigwa mpaka kufa,watu wasiopungua watatu wamenyongwa na wengine wamepigwa risasi na kufa baada ya kukamatwa au kusalimu amri, ripoti ya Amnesty International imesema.

Hata hivyo shirika hilo linahisi uhalifu uliofanywa na wanamgambo huo ni "mdogo" ukililinganishwa na ule uliofanyika wakati wa utawala wa Muammar Gaddafi wanaosema huenda wakabebeshwa dhamana ya uhalifu dhidi ya ubinaadam.

Libyen Kämpfen in Bani Walid

Wapiganaji wanajiandaa kuingia Bani Walid

Katika hotuba yake ya kwanza tangu alipofika Tripoli, kiongozi wa mpito wa Libya, Mustafa Abdel Jalil, amewaambia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika katika Uwanja wa Mashahidi kwamba uislamu wa wastani ndio msingi wa sheria ya Libya.

"Hatutoridhia nadharia kali yoyote, si ya mrengo wa kulia na wala si ya mrengo wa shoto. Sisi ni waislam, itikadi ya wastani na tutafuata njia hiyo hiyo." Amesema Mustafa Abdel Jalil.

Wakati huo huo baraza la mpiito la taifa linaendelea kumsaka Muammar Gaddafi ambaye vikosi vyake vinaendelea kupigana katika miji minne ikiwa ni pamoja na mji alikozaliwa wa Sirte na Bani Walid.

Mamia ya watu wanaupa kisogo mji huo uliopo umbali wa kilometa 150 kusini mashariki ya Tripoli.

"Uwanja wa nyumba yetu umehujumiwa. Hatuwezi tena kuvumilia. Watoto wanaogopa kweli kweli."

Libyen Tripolis Aufständische suchen weiter nach Verwandten von Muammar al Gaddafi

Wanamgambo wanamsaka Muammar Gaddafi

Gaddafi anayesakwa na korti ya kimataifa ya uhalifu kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinaadam, hajulikani aliko. Katika taarifa iliyosomwa na televisheni ya Syria, Muammar Gaddafi ameapa kuwavunja nguvu wale waliompindua. Hata jumuiya ya kujihami ya NATO inasema haina habari wapi alikojificha Gaddafi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com