1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LIBYA : Pande hasimu zasusia mazungumzo ya Geneva

Saleh Mwanamilongo
25 Februari 2020

Pande mbili zinazohasimiana nchini Libya zimetangaza kusitisha mazungumzo ya amani ya Geneva.Hata hivyo UN inayo suluhisha mzozo huo wa Libya umelezea kwamba tarehe ya kuanzishwa tena kwa mazungumzo hayo haitobadilishwa.

https://p.dw.com/p/3YNFl
Wamajeshi wa serikali ya muungano wa kitaifa ya mjini Tripoli
Wamajeshi wa serikali ya muungano wa kitaifa ya mjini TripoliPicha: picture-alliance/Photoshot/H. Turkia

Pande mbili zinazohasimiana nchini Libya zimetangaza kusitisha mazungumzo ya amani ya mjini  Geneva, kila upande ukitoa sababu zake. Hata hivyo Umoja wa Mataifa unao suluhisha mzozo huo wa Libya umelezea kwamba tarehe ya kuanzishwa tena kwa mazungumzo hayo haitobadilishwa. 

Upande unaomuunga mkono jenerali Khalifa Haftar anayelidhibiti eneo la Mashariki mwa Libya umetangaza kwamba hautoshiriki kwenye mazungumzo hayo kwa sababu umoja wa mataifa haukuwashirikisha wajumbe wake wote 13.

Kwa upande wake, serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini Tripoli ilielezea kwamba  inasubiri matokeo ya mazungumzo ya kijeshi kabla ya kushiriki kwenye mazungumzo hayo ya kisiasa mjini Geneva.

Taarifa yake ilisema ni kufuatia matokeo hayo ya mazungumzo ya kijeshi ndio serikali hiyo itamua ikiwa itashiri kwenye mazungumzo hayo au la.

Hata hivyo msemaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Jean El Alam, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba , mazungumzo ya kisiasa ya Geneva, yataendelea kama ilivyopangwa, na kuthibitisha kwamba wajumbe walioalikwa watahudhuria mkutano huo.

Mwito kwa ajili ya utawala wa kiraia

Akikosoa mashambulizi ya hivi karibuni ya mjini Tripoli na vikosi vya jenerali Haftar, kwenye kikao cha tume ya haki za binadamu ya umoja wa mataifa , waziri mkuu wa serikali ya mjini Tripoli Fayez Sarraj amesema kwamba kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba haki za binadamu ni lazima ziheshimiwe na Libya inatakiwa kuwa taifa la haki.

Rais wa Uturuki  Recep Tayyip Erdogan (R) na waziri mkuu wa serikali ya muungano wa taifa nchini Libya, Fayez Al Sarraj
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (R) na waziri mkuu wa serikali ya muungano wa taifa nchini Libya, Fayez Al Sarraj Picha: picture-alliance/AP Photo/Turkish Presidency

'' Hatuwezi kukubali kurejea kwa uongozi wa kidikteta na wa kijeshi. Tunatoa mwito wa kuweko na utawala wa kiraia na wa kidemokrasia.Tunatowa mwito wa kuweko na uchaguzi'' alisema Sarraj.

'' Lakini vita hivyo vya makundi hasimu vinavyoendelea kwenye ardhi  ya Libya vinatakiwa kumalizika, na hiyo ni majukumu ya jumuiya ya kimataifa na moja wapo  ya masharti kwa raia wetu'' aliendelea kusema  Fayez Sarraj.

Tume ya pamoja ya kijeshi yenye wajumbe 10 kuta kwenye pande zote mbili hasimu, ilikutana hadi Jumapili mjini Geneva na ilifikia hatua ya kueko na mkataba wa usitishwaji mapigano ambao mkataba huo utakamilika mwezi machi, kwa mujibu wa umoja wa mataifa.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alitangaza leo kwamba wanajeshi wawili wa nchi yake waliuliwa mjini Tripoli,lakini hakufahamisha lini na katika mazingira gani wanajeshi hao waliuliwa. Uturuki ilipeleka wanajeshi wake kuunga mkono serikali ya Tripoli dhidi ya mashambulizi ya jenerali Khalifa Haftar.