1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liberia: rasimu ya sheria kwa ajili ya mahakama ya uhalifu

Saleh Mwanamilongo
25 Juni 2021

Asasi za kiraia nchini Liberia zawasilisha rasimu ya sheria bungeni ili kuundwa korti ya uhalifu nchini humo miaka 20 baada ya vita vya wenyenye kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/3vZlV
Äthiopien Addis Abeba Afrikanische Union Gipfel Guterres George Weah
Picha: Reuters/T. Negeri

Takriban watu 250,000 waliuawa mnamo kipindi cha miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia. Lakini ni wachache miongoni mwa waliohusika na uhalifu huo ambao wamefikishwa mahakamani.

Nchini Liberia kwenyewe hakuna aliyeshitakiwa hadi sasa kutokana na uhalifu huo, kwa sababu washukiwa bado ni wenye nguvu na wenye madaraka. Chama cha mawakili na asasi za kiraia yakiwemo makundi ya kidini, mashirika ya wanafunzi na yale ya wanawake wamewasilisha bungeni rasimu ya sheria ili kuundwa mahakama ya uhalifu nchini humo.

Tiawon Gongloe, Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Liberia amesema ni lazima nchi hiyo kuiga mfano wa nchi nyingine.

''Hatuko peke yetu, Sierra Leone na Rwanda zilimaliza vita vyao. Kufuatia hali hiyo ulimwengu uliziamini nchi hizo mbili na hivi sasa hazichukuliwi tena kama mataifa dhaifu. Na nchi hizo zimetembelewa na kumekuwa na uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje.'',aliendelea kusema Gongloe. 

Gongloe amewaambia waandishi habari jijini Moronvia kuwa wamewasilisha nakala 176 ya rasimu hiyo ya sheria , sawa na idadi ya jumla ya wabunge wa Liberia.

Rasimu ya sheria hiyo imependekeza kuweko na kesi kwa ajili ya washukiwa wakuu wa uhalifu pamoja na wababe wakivita. Moja wao akishikilia hivi sasa wadhifa wa juu kwenye baraza la Seneti la nchi hiyo.

Hatua ya kimaadili

Liberia Wahlen 2016 Anhänger DCC Partei
Picha: picture-alliance/dpa/A. Jallanzo

Mwezi Mei, Prince Johson alichaguliwa kuongoza kamati ya Seneti ya ulinzi na usalama, hatua iliyokosolewa vikali na Marekani.

Wakati huo huo, kesi kadhaa dhidi ya makamanda wa zamani zinaendelea kusikilizwa nchini Finland, Ufaransa na Uswisi.

Suala la kuundwa kwa korti ya uhalifu nchini Liberia lilimulikwa pia wakati wa kikao cha kamati ya bunge la Marekani inayoshughulikia masuala ya kigeni.

Jeremiah Swen, Katibu Mkuu wa Asasi za kiraia nchini Liberia amesema ikiwa serikali itashindwa kuunda mahakama hiyo, basi washukiwa watawajibishwa na taasisi za kimataifa.

''Kuna vyombo vingi vya kimataifa vya kupambana na uhalifu vinayoweza kutumiwa,lakini njia muafaka ni Liberia kufanya hivyo kimaadili.'',alisema Swen.

Juni 18, Mahakama ya uhalifu ya shirikisho nchini Usiwsi ilimuhukumu kifungo cha miaka 20 jela mbabe wa zamani wa kivita nchini Liberia, Alieu Kosiah, na kuwa mtu wa kwanza kutoka kwenye taifa hilo kuhukumiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita yaliyofanywa wakati wa mzozo mbaya kabisa kati ya mwaka 1989 na 2003. Liberia ilitumbukia mara mbili kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2003.