Liberia kufanya uchaguzi wa duru ya pili | Matukio ya Afrika | DW | 24.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Liberia kufanya uchaguzi wa duru ya pili

Waliberia watamchagua kiongozi mpya Jumanne (27.12.2017) katika uchaguzi wa duru ya pili kati ya makamu wa rais Joseph Boakai na mchezaji kandanda wa zamani maarufu George Weah.

Kura hiyo itaashiria mabadiliko  ya  kwanza  ya uongozi  nchini  humo  tangu  mwaka  1944.

Baada ya wiki saba za uchelewesho kutokana na malalamiko ya kisheria  yaliyofikishwa  mahakamani  na  chama  tawala  cha Boakai cha Unity dhidi ya tume ya uchaguzi nchini humo, vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi  saa za Liberia na kufungwa majira ya saa 12  jioni kwa ajili ya wapigakura milioni 2.1 waliandikishwa kupiga kura.

Chama  cha  Weah cha  Muungano  kwa  ajili  ya  mabadiliko  ya kidemokrasi, Coalition for Democratic Change (CDC) kimewataka wapiga  kura  kutokunywa  pombe kupita  kiasi  katika  sikukuu  ya Krismasi na  kuamka  mapema  siku  ya  tarehe  26  kupiga  kura zao  katika  kile  mwenyekiti  wa  tume  ya  uchaguzi  ya  taifa  NEC, Francis Korkoya  alichosema  kuwa  ni "kujitolea  mhanga  kwa  ajili ya demokrasia  yetu  na  nchi  yetu."

Watachagua  mrithi  wa  rais Ellen Johnson Sirleaf, anayetarajiwa kuondoka  madarakani  mwezi  Januari  baada  ya  miaka  12 akiwa katika uongozi  wa  juu  wa  taifa  hilo  la  Afrika  Magharibi, linaloibuka  kutoka  katika  mavumbi  ya  vita  vya  wenyewe  kwa wenyewe,(1989-2003) na pia kushughulikia hatua za kupambana  na mzozo  wa  ugonjwa  wa  Ebola (2014-16).

George Weah (Chris Hondros/Getty Images)

Mchezaji soka wa zamani Goerge Opuku Weah mgombea urais Liberia

Duru  ya  kwanza

Katika  duru  ya  kwanza  ya  upigaji  kura  tarehe 10 Oktoba, Weah alipata   asilimia  38.4  ya  kura  wakati  Boakai  alikuwa  wa  pili akipata  asilimia  28.8, na  kuzusha  hatua  ya  duru  ya  pili  ya uchaguzi  kwa  kuwa  hakuna  kati  ya  wagombea  hao  wawili aliyeweza  kufikisha  idadi  ya  asilimia  50  ya  kura  inayohitajika kushinda moja  kwa  moja.

"Matokeo  yatakuwa yanakaribiana  sana,"  amesema  Ibrahim Al-Bakri Nyei, mchambuzi  wa  masuala  ya  siasa  nchini  Liberia katika  shule  ya  mitaala ya  masuala  ya  mashariki  ya  kati  na Afrika  katika  chuo  kikuu  mjini  London (SOAS), akisema  Weah alikuwa  katika  nafasi  kama  hiyo  katika  uchaguzi  wa  mwaka 2005  wakati  aliposhindwa  licha  ya wengi  kutabiri kwamba atashinda. Kutokana  na  siku  ya  uchaguzi, "inawezekana  kuwapo idadi  ndogo  ya  watu watakaopiga  kura  kuliko uchaguzi  wa kwanza,"  alitabiri.

Akisifu mchakato  usiokuwa  na  ghasia  wa  uchaguzi  hadi  sasa, Sirleaf  alisema  katika  hotuba  yake  hivi  karibuni  kwamba "uchaguzi  umechukua  nafasi  ya  risasi na mizozo  ya  uchaguzi inatatuliwa kupitia  mahakama", ikiwa  ni  ishara  ya umbali  gani Liberia  imetoka  tangu  wakati  wa  vita.

Mahakama haikuweza kuthibitisha mapungufu

Chama  cha  Unity  cha  Boakai kimejiunga  na  chama  cha  upinzani cha  Liberty kupambana  na  kile  alichosema "mapungufu  makubwa na  udanganyifu" katika  matokeo  ya  uchaguzi, lakini  mahakama kuu iligundua  kuwa  madai  hayo  hayakuweza  kuthibitishwa, na waangalizi  walitangaza  kuwa  uchaguzi  huo  ni  wa  kuaminika.

Vizepräsident Joseph Nyuma in Monrovia Liberia (Reuters/T. Gouegnon)

Makamu wa rais wa Liberia Joseph Nyuma Boakai

Jaribio  la  mwisho  kuzuwia  kura  hiyo  na  kukabidhi  majukumu  ya kutangaza  tarehe  mpya  kwa  bunge lilikataliwa  siku  ya  Alhamis na  mahakama  hiyo  ya  juu  nchini  humo. Wakati  huo  huo juhudi za  kuvutia kuungwa  mkono  kutoka  kundi  la  wagombea  wengine 18  walioshindwa  katika  kinyang'anyiro  hicho  katika  duru  ya kwanza  imeishia  katika kupata wagombea  wachache  wasio  na uhakika  licha  ya  Weah  kuidhinishwa  na  mbabe  wa  kivita aliyejibadilisha  kuwa  mchungaji Prince Johnson, ambaye  ni maarufu sana   katika  kaunti  yenye  wakaazi  wengi  ya  Nimba.

Mwanasoka  huyo  wa  zamani  Weah  pia  alipigwa  picha  katika tukio  la  hadhara  pamoja  na  Sirleaf siku  ya  Alhamis, akikoleza uvumi kwamba  rais  huyo mstaafu  anaweza  kumuidhinisha  dhidi ya  makamu  wa  rais  aliyetumika  nae  kwa  miaka  12. Weah  pia alipata  kura  nyingi  katika  kaunti  ya  Bong, ngome  ya  mbabe  wa kivita  wa  Liberia  rais  wa  zamani  Charles Taylor  na  mkewe  wa zamani , Jewel Howard-Taylor, ambaye  ni makamu wa  rais aliyeteuliwa  na  mwanasoka  huyo wa  zamani. Charles Taylor kwa sasa  anatumikia  kifungo  cha miaka 50  nchini  Uingereza kwa uhalifu  aliofanya katika  nchi  jirani  ya  Sierra  Leone, lakini ushawishi  wake  bado  upo katika  uchaguzi  huo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com