1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lewandowski miongoni mwa washindi tuzo ya Laureus

25 Aprili 2022

Baada ya kuinyakua tuzo ya mchezaji bora duniani ya FIFA Best, mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski amenyakua tuzo ya Laureus katika kitengo cha Mafanikio Makubwa zaidi.

https://p.dw.com/p/4APs8
Fußball Bundesliga | Bayern München v Borussia Dortmund
Picha: Revierfoto/IMAGO

Hii ni baada ya kuivunja rekodi ya ufungaji magoli iliyowekwa na mkongwe wa Bayern Munich Gerd Müller ya magoli 41 iliyodumu kwa miaka 49.

"Nashukuru sana kwa kutambulika na watu wazuri kama nyie, wanariadha na wakongwe kutoka ulimwengu mzima wa michezo. Hakuna njia za mkato katika mafanikio michezoni, iwapo unataka kuwa bora ni sharti ujitahidi ila naamini pia kwamba hakuna mchezaji anayeweza kupata mafanikio pekeyake na ndio maana nataka kumshukuru kila mmoja anayeniunga mkono. Nelson Mandela alisema, 'michezo ina nguvu ya kuubadilisha ulimwengu,' kwa hiyo tuukumbuke ujumbe huu na tuurudie kwa nguvu hasa wakati huu ambao watu wasio na hatia wanafariki nchini Ukraine," alisema Lewandowski.

Tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka ilimwendea bingwa wa magari ya langa langa ya Formula One Max Verstappen huku Elaine Thompson-Herah akitajwa kama mwanamichezo bora upande wa wanawake.

Formel 1 Imola | Red Bull Max Verstappen
Derreva wa Red Bull Max VerstappenPicha: HochZwei/IMAGO

Verstappen amenyakua tuzo hiyo baada ya kushinda taji la kwanza la Formula kwa kumshinda Lewis Hamilton ambaye ni bingwa mara saba katika mashindano ya mwaka jana huko Abu Dhabi.

Elaine Thompson-herah naye amenyakua tuzo ya mwanamichezo bora kwa wanawake baada ya kushinda dhahabu katika mbio za mita mia moja na mita mia mbili kwenye mashindano ya Olimpiki huko Tokyo, Japan mwaka uliopita.

Tokio 2020 | Leichtathletik | Elaine Thompson-Herah
Bingwa wa Olimpiki mbio za mita 100 na 200 Eilaine Thompson-HerahPicha: David Goldman/AP Photo/picture alliance

Mchezaji tennis wa Uingereza Emma Raducanu naye alishinda tuzo ya mwanamichezo chipukizi baada ya ushindi wake wa mashindano ya Grandslam ya US Open mwaka uliopita.