Leverkusen yaingia Champions League kwa kishindo | Michezo | DW | 28.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Leverkusen yaingia Champions League kwa kishindo

Baada ya kuweka rekodi ya kufunga goli la kasi zaidi katika Bundesliga, la sekunde 9 dhidi ya Borussia Dortmund, Leverkusen ilihitaji tu sekunde 70 kufungua la kwanza dhidi ya FC Copenhagen.

Son Heung-min alitikisa wavu kwa mguu wake wa kushoto, baada ya kuandaliwa pasi safi kutoka kwa Stefan Kiessling, na kuimarisha nafasi ya klabu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kufuatia ushindi wake wa magoli matatu kwa mawili waliopata wiki iliyopita nchini Denmark.

Mkwaju wa free kick wake Hakan Calhanoglu, ambao ulielekezwa langoni baada ya kumgonga mchezaji wa Copenhagen na kumwacha kipa Stephen Anderson kama mtazamaji tu, lilifanya mambo kuwa mawili kwa Leverkusen katika dakika saba tu na kuua kabisa matumaini ya timu hiyo ya Denmark kujaribu kupambana.

Champions League Qualifikation Leverkusen vs Kopenhagen Stale Solbakken

Kocha wa FC Copenhagen Stale Solbakken alikuwa na usiku mrefu kwa kushuhudia kichapo

Leverkusen wamekuwa na mwanzo mzuri wa msimu chini ya kocha mpya Roger Schmidt, baada ya kupenya katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani – DFB, wakaibwaga Borussia Dortmund magoli mawili kwa sifuri katika siku ya ufunguzi wa msimu, na sasa kujinyakulia mamilioni ya euro za Champions League kwa msimu huu. Stefan Kiessling amekuwa moto wa kuotea mbali na alifunga la tatu kwa njia ya penalti.

Leverkusen walipinguza kasi katika kipindi cha pili na kuwapa nafasi Copenhagen kujaribu kushambulia lakini hawakufua dafu. Kiessling kisha alibusu wavu kwa mara nyingine na kuhitimisha kichapo hicho cha magoli manne kwa sifuri. Ina maana kuwa klabu hiyo ya Ujerumani imefuzu kwa jumla ya magoli saba kwa mawili. Leverkusen sasa imejiunga na vilabu vingine vya Ujerumani Bayern Munich, Schalke na Borussia Dortmund katika timu 32 za awamu ya makundi.

Timu nyingine zilizofuzu jana ni Arsenal, Malmo, Athletic Bilbao, Ludogorets, Zenit St Petersburg, BATE Borisov, Maribor, APOEL Nicosia na Porto. Droo ya mechi za makundi itafanyika hii leo jioni mjini Monaco. Droo ya awamu ya makundi inafanyika leo mjini Monaco.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Josephat Charo