1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lesotho na Umaskini baada ya kukosa kuondolewa madeni na G8

15 Juni 2005

Kiwango cha Umaskini nchini Lesotho ni kikubwa kutokana na makampuni mengi ya nguo kufunga biashara kufuatia ushindani mkubwa kutoka mataifa ya Asia

https://p.dw.com/p/CHgT

Ikiwa ni nchi iliyomo ndani ya umaskini mkubwa,Lesotho ni mojawapo kati ya nchi zenye madeni makubwa ambazo hazikutajwa katika mpango wa nchi nane tajiri duniani wa kutoa nafuu ya mzigo wa madeni kwa mataifa hayo.

Waziri wa fedha wa Lesotho Timothy Thahane anasema nchi hiyo haikutambulika tu kwenye mpango huo bali pia haijatambulika kwenye mpango wa kuondosha vizingiti vya biashara huru.

Kumalizika kwa mkataba wa kimataifa unaohusu viwango vya usafirishaji wa bidhaa miongoni mwa mataifa mbali mbali ambako kulipunguza uzalishalishaji wa bidhaa katika mataifa ya Asia,,kulisababisha kufungwa kwa viwanda vingi nchini Lesotho.Nchi hiyo iliyozungukwa na Afrika Kusini ilishindwa kushindana kibiashara na China kutokana na kuwa China inazalisha kwa wingi bidhaa zake.

Waziri huyo wa fedha wa Lesotho aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba kumalizika kwa mkataba huu kuliitumbukiza nchi yake kwenye ushindani mkali wa kibiashara na mataifa kama vile China India na Bangladesh. Aliendelea kusema kuwa sasa wafanyibiashara wa nguo nchini humo wanalazimika kushindana na makampuni bora zaidi yaliyoimarika kibiashara.

Waziri huyo anasema nchini Lesotho makampuni mengi yameathirika na hivyo kusababisha kazi nyingi kupotea na makampuni mengi kufunga biashara,hasa makampuni madogo madogo ya nguo ambayo aghalabu yanamilikiwa na China na Taiwan.

Hata hivyo waziri huyo wa fedha anasema Lesotho inapigania kupata mipango mizuri ya kibiashara na wafanyibiashara wa mataifa ya magharibi.

Katika sehemu za viwandani mjini Maseru,viwanda na maduka yaliyoko karibu ambayo yalikuwa yakiuza vyakula wakati wa mchana kwa wanaofanyakazi yamebakia wazi bila ya wauzaji kutokana na kufungwa kwa makampuni mengi huku wafanyikazi wa zamani wakisubiri nje ya makampuni yaliyosalia wakitumai angalau kupata ajira.

Kama anavyosema kijana Matselisto Lebetla mwenye umri wa miaka 25,anasema yeye kila asubuhi hufika mahala hapo kutafuta ajira.Matselisto alikuwa akituma kiasi cha dola 94 kila mwezi kijijini kwao huko Lesotho ya kati lakini sasa hana tena ajira na anasema kila anapofika anaambiwa hakuna kazi na hakuna anayewaeleza sababu,ilicho bakia ni kukaa na kusubiri tena kudura ya mwezi mungu.

Huku kila mfanyikazi nchini humo akiwa anaangalia familia ya watu watano au zaidi, hali inazidi kuwalemea, kwani hakujakuwepo na mazao ya kutosha nchini katika kipindi cha miaka mitano. juu ya hayo asilimia 30 ya watu nchini humo wameambukizwa virusi na maradhi ya ukimwi na kusababisha idadi ya watu milioni mbili nchini humo kutegemea chakula cha msaada.

Viwanda pia nchini humo vimeathirika kutokana na kuongezeka kwa thamani ya fedha ya Afrika kusini RAND na pamoja na kumalizika kwa mkataba wa AGOA nchini Marekani ambao ulikuwa unairuhusu Lesotho kuuza nguo zao kama vile Jeans na Tshirt au fulana nchini Marekani kwa bei nafuu kuliko washindani wao wa kibiashara wa Asia.

Kwa mujibu wa bwana Thahane ili nchi hiyo iweze kupanua uchumi wake lazima kuwepo na usaidizi wa kutoka nje lakini vyombo vya habari nchini humo vinasema ukosefu wa ajira ni asilimia 50 lakini hakuna kiwango kamili kilicho tolewa .Upande wao wachunguzi wa mambo wanasema kilichosalia sasa kuwa tumaini la pekee kwa nchi hiyo ni madini,utalii na kilimo cha kisayansi.

Thahane anasema nchi hiyo ikiondolewa asilimia 85 ya madeni yake ambayo yanafikia dola milioni 600 kwa wakopeshaji wa kimataifa kama vile shirika la fedha la kimataifa na benki ya dunia huku ikiwa ina deni jingine la asilimia 15 kwa nchi ya Ufaransa na Afrika kusini itaiwezesha kutumia kiasi kilichobaki katika kupunguza kiwango cha umaskini nchini humo.