Leo ni zamu ya Kombe la ligi la Ulaya | Michezo | DW | 08.04.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Leo ni zamu ya Kombe la ligi la Ulaya

Baada ya kupigwa kumbo jana Manchester United na Bayern Munich nje ya champions league - na Munich kuweka miadi na Olympique Lyon ya Ufaransa kwa nusu-finali ya kombe hilo

Edin Dzeko wa VFL Wolfsburg kushoto-mzinga hatari.

Edin Dzeko wa VFL Wolfsburg kushoto-mzinga hatari.

Leo ni zamu ya klabu 2 nyengine za Ujerumani kuteremka viwanjani jioni hii kuwania nafasi ya nusu finali ya Kombe la Ligi la Ulaya, zamani Kombe la UEFA.

Mabingwa wa Ujerumani VFL Wolfsburg, wana miadi na FC Fulham ya Uingereza. Hamburg, imeitembelea Liege ya Ubilgiji .

Kwa kinyan'ganyiro cha usiku wa leo cha Kombe la Ligi la Ulaya, matumaini yako juu kwa mabingwa wa Ujerumani, Wolfsburg kama vile mwaka jana walipotwaa ubingwa wa Bundesliga. Mashabiki wao nyumbani , wameingiwa na hamasa kuu wakisubiri firimbi tu kulia ili mizinga yao 2 mikali-mbrazil Grafite na mbosnia Edin Dzeko, iliokwishanolewa makali ianze hujuma. FC Fulham, yabidi kuchunga hapo , manuwari yao kutoka Uingereza, isizamishwe nyumbani mwa kiwanda cha motokaa cha VW.

Wolfsburg imejiwinda kufuta mabao 2:1 iliokandikwa na Fulham duru ya kwanza na mbwamwitu wa Wolfsburg, wameapa kutoliachia jogoo la shamba Fulham kuwika leo mjini Wolfsburg.

Timu ya pili ya Ujerumani, inayoteremka uwanjani ni Hamburg ambayo kama Fulham, ilishinda duru ya kwanza mabao 2:1 nyumbani Hamburg. Ikitamba na stadi wao kutoka Holland -van Niestelrooy, Hamburg imewachimbia kaburu Liege uwanjani kwao na imepanga kuwazika wahayi firimbi ya mwisho ikilia jioni hii na kuwapa mkono wa buriani wakiaga nao kama Manu jana,Kombe jengine la Ulaya.

Nani atasahau changamoto ya jana usiku huko Old Traford? Bila ya shaka sio Manu. Kwani, pamoja na mzinga wao waliouficha kichakani, Wayne Rooney, hawakufua dafu mbele ya mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani Bayern Munich. Hata vishindo vyao vya kipindi cha kwanza vilivyowapatia mabao 3 ya haraka: la kwanza kutoka kwa Darron Gibson na 2 maridadi ajabu kutoka kwa Nani, hayakutosha jana kuzuwia msumari wa mwisho kupigwa na mdachi Arjen Robben katika jeneza lao na kuaga champions league msimu huu.

Ilionekana kana kwamba, Manu ilifyatua risasi zake zote na mapema na pale Olic alipolifumania lango la kipa van der Sar kwa bao la kwanza la Munich, vishindo vya Manu na mashabiki wao Old Traford vilianza kufifia. Kwa kutolewa nje ya chaki ya uwanja kwa Rafael alietamba sana kwa Manu na rifu kwa mchezo wake wa ngware, hatima ya Manu ilionekana imeshakatwa.

Ni Bayern Munich na sio Manu, itayocheza nusu-finali na Olympique Lyon wakati mabingwa FC Barcelona na mchawi Messiah wao Lionel Messi, watachuana na Real Madrid. Je, huu ni mwaka mwengine wa Bayern Munich au wa Barcelona? Na turufu gani wanazo Lyon na Inter Milan?

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE/EXP.

Uhariri: Josephat Charo