1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni miaka kumi tangu Princes Diana alipoaga dunia

31 Agosti 2007

Ndugu, jamaa na marafiki leo waliungana pamoja na wana mfalme William na Harry katika kanisa la Guards mjini London karibu na Kasri la Buckingham kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 10 tangu Princes Diana alipofariki.

https://p.dw.com/p/CB1c
Marehemu Princes Diana wa Uingereza
Marehemu Princes Diana wa UingerezaPicha: AP

Prince William mwana wa kwanza wa marehemu Princes Diana alinukuu kifungu cha maneno kutoka kwenye waraka wa mtakatifu Paul kwenye kitabu cha Ephisians mstari wa tatu unaohimiza imani ya hali ya juu.

ibada hiyo maalum ilihudhuriwa na jamii ya malkia Elizabeth wa Uingereza akiwemo Prince Philip na Prince Charles pamoja na jamaa na marafiki.

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown na mawaziri wakuu waliomtangulia Tony Blair na John Major walikuwepo pia katika kumbukumbu hiyo.

Mke wa Prince Charles bibi Camila Parker hakuhudhuria kumbukumbu hiyo, ametoa sababu na kusema kuhudhuria kwake kungechanganya mawazo katika shughuli hiyo.

Askofu Patrick Irwin aliwahutubia takriban waumini 500 waliokusanyika kanisani.

Prince Harry mwana mdogo wa marehemu Princes Diana, alitoa ushuhuda na kumtaja marehemu mama yake kwamba wakati wa uhai wake alikuwa chachu ya furaha kwa familia yake pamoja na watu wengine kadhalika.

Prince Harry aliongeza kusema kwamba kifo cha mama yake kilimshitua na kinamsikitisha mbali na kubadili maisha yake.

Kumbukumbu hiyo ilitawaliwa na nyimbo alizozipenda Princes Diana ikiwa ni pamoja nyimbo inayoitwa, I Vow To Thee My Country iliyoimbwa na wanakwaya wa London Westminster, Abbey.

Awali mfanya biashara tajiri mjini London Mohamed Al Fayed baba yake Dodi Fayed aliyekuwa mpenzi wa Prices Diana kabla wote kufa katika ajali aliweka shada la maua mahali alipopajenga kwa heshima ya marehemu hao na kutulia kimya kwa dakika mbili.

Hadhi ya familia ya kifalme imeshuka kwa kiwango cha asilimia 50 kufuatia kifo cha Princes Diana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kumi.

Matokeo ya kura ya maoni yameonyesha kuwa wananchi nchini Uingereza hawana imani na familia ya kifalme kuwa imebadilika na kujiimarisha tangu kifo cha Princes Diana miaka kumi iliyopita.