1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo mei tatu ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

2 Mei 2007

Mwaka 2006 watajwa kuwa mwaka mbaya kwa wandihsi habari 100 waliuwawa huku Ethiopia ikiongoza katika ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari

https://p.dw.com/p/CB4M

Ripoti ya Mwaka 2006 ya Taasisi ya habari ya mjini Vienna imeeleza kuwa waandishi habari kiasi 100 waliuwawa.

Kwa upande mwingine kamati ya kutetea waandishi habari ya Marekani CPJ imezitaja nchi 10 zinazoongoza katika ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari.Ethiopia inaongoza kwenye orodha hiyo.

Mwaka 2006 ni mwaka uliotajwa kuwa mbaya kabisa katika historia ya vyombo vya habari duniani ambapo wanahabari 100 waliuwawa.

Idadi hiyo imetokana na kulengwa kwa waandishi wa habari nchini Iraq ambapo 46 waliuwawa nchini humo. Mbali na tathmini hiyo iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya habari ya mjini Vienna kamati ya kutetea wandishi habari yenye makao yake Marekani imetoa ripoti yake ambayo imezitaja

Nchi 10 zinazoongoza katika ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari. Nchi hizo ni Ethiopia,Gambia,Urussi,Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo Cuba,Pakistan,Misri,Azerbaijan,Morrocco na Thailand. Mkurugenzi mtendaji wa kamati hiyo Joel Simon amesema hali ya wandishi habari kwenye nchi hizi inatia mashaka lakini mabadiliko katika nchi ambako vyombo vya habari vimestawi yanaonyesha ni jinsi gani haki msingi ya uhuru wa kujieleza unavyoweza kuondolewa.

Ethiopia inaongoza kwenye orodha ya nchi zinazokandamiza uhuru wa vyombo vya habari ambapo idadi ya wanahabari waliofungwa nchini humo imepanda kutoka wawili hadi 18 na wengi wameomba hifadhi kwenye nchi nyingine kati ya mwaka 2002 hadi 2007.

Kamati ya kutetea wandishi habari ya CPJ imesema magazeti nane yalifungiwa na wandishi wawili wa kigeni walifurushwa nchini humo na tovuti kadhaa kuzuiwa.

Nchini Gambia mwandishi habari mashuhuri Deyda Hydara alipigwa risasi na kuuwawa mwaka 2004 na gazeti linalosomwa na wengi la ‘’Independent’’ lilitiwa moto na baadae kufungiwa na serikali. Urussi imeorodheswa ya tatu kwasababu vituo vyote vitatu vya televisheni vinaendeshwa na serikali na wandishi habari 11 waliuwawa katika kipindi cha miaka mitano na hakuna kesi hata moja kati yazo iliyoshughulikiwa.

Nchini Kongo wandishi habari wawili waliuwawa mwaka 2005, Idadi ya wandishi wa habari walioshambuliwa imeongezeka kutoka watatu hadi tisa na viongozi wa kundi la kutetea uhuru wa vyombo vya habari nchini humo walilazimika kujificha mwaka 2006.

Wakati huo huo ripoti ya mwaka ya taasisi ya kimataifa ya habari ya mjini Vienna inasema katika nchi za Libya Saudi Arabia na Syria unaweza kusema hakuna kabisa uhuru wa vyombo vya habari.

Barani Asia wandishi habari 29 waliuwawa kumi kati yao nchini Ufilipino. China nayo inadhibiti shughuli za Internet kwa usaidizi wa mashirika ya kimataifa na matumizi ya nguvu dhidi ya waandishi habari yameongezeka nchini humo ambapo tayari wandishi habari wawili wameuwawa

Wanahabari wane waliuwawa huko Pakistan na utekaji nyara unashuhudiwa mara kwa mara na waandishi .

Nchini Zimbabwe sheria ngumu zimevisakama vyombo huru vya habari.

Hali pia sio nzuri nchini Kenya na Nigeria ambako vyombo kadhaa vya habari vilivamiwa na polisi wa serikali.