1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lejendari wa Ujerumani Jürgen Grabowski afariki

11 Machi 2022

Mashabiki wa soka hapa Ujerumani wanaomboleza kifo cha lejendari wa timu ya taifa ya Ujerumani na mshindi wa kombe la dunia la mwaka 1974 Jürgen Grabowski aliyefariki akiwa na umri wa miaka 77.

https://p.dw.com/p/48NA0
Fußballspieler Jürgen Grabowski gestorben
Picha: Andreas Arnold/dpa/picture alliance

Mke wa Grabowski ameliambia shirika la habari la dpa kuhusu kifo cha mumewe aliyefariki hospitalini siku ya Alhamisi.

Kiungo huyo aliichezea timu ya taifa ya Ujerumani Magharibi mechi 44 na alishinda kombe la Ulaya mnamo mwaka 1972 kabla ya kushinda kombe la dunia miaka miwili baadaye.

Katika mechi ya fainali, ambapo Ujerumani Magharibi iliifunga Uholanzi 2-1, ilichezwa siku yake ya kuzaliwa ambapo Grabowski alikuwa anatimiza miaka 30.

Grabowski aliichezea Frankfurt maisha yake yote ya soka, akiichezea mechi 441 za ligi kuu ya Bundesliga. Akiwa Frankfurt, alishinda kombe la Ulaya la UEFA mnamo mwaka 1980 na kombe la Ujerumani mara mbili, mwaka 1974 na 1975.

Rais wa klabu ya Eintracht Frankfurt Peter Fischer ameuambia mtandao wa klabu hiyo, "Jürgen Grabowski alikuwa na uwezo mkubwa wa kutoa pasi. Alikuwa mchezaji hodari kwetu."

Mkurugenzi mtendaji Axel Hellman pia alimmiminia sita tele nahodha huyo wa zamani, "Mchezo wake utasalia kumbukumbu hadi leo. Grabi, kama alivyojulikana kwa jina la utani, atasalia mfano wa kuigwa kwenye klabu hiyo kwa vizazi vijavyo."