Lebanon: Hariri asitisha kujiuzulu kwake | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Lebanon

Lebanon: Hariri asitisha kujiuzulu kwake

Waziri Mkuu wa Lebanon Saad al Hariri amesitisha uamuzi wake wa kujiuzulu baada ya kurejea nchini kwake na kushiriki gwaride la Siku ya Uhuru,

Muda mfupi  baada ya kurejea mjini Beirut, Hariri alikutana na Rais Michel Aoun, ambaye tangu mwanzo alikataa kukubali kujiuzulu kwa waziri huyo mkuu, akimtaka kwanza arejee nyumbani Lebanon. Na katika hotuba yake mbele ya umati mkubwa wa wafuasi wake waliokusanyika nje ya nyumba yake katika mji wa Beirut, Hariri aliahidi kuwa atabakia nchini Lebanon ili kulinda utulivu wa nchi hiyo.

Waziri mkuu wa Lebanon Hariri akiwaili kwenye sherehe za uhuru (Reuters/M. Azakir)

Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri

Hariri aliwaambia wafuasi wake kwamba alipowasilisha waraka wake wa kujiuzulu, rais alimwomba afanye subira ili kwanza kufanyike mashauriano zaidi kutokana na sababu zake na pia kwa kutazama historia ya kisiasa. Hariri alikubali ombi la rais Aoun.  Amesema ana matumaini kuwa yataanzishwa majadiliano ambayo yatazingatia Mkataba wa Taif na msingi wa makubaliano ya kitaifa, ambayo pia yatazingatia masuala ya kutofautiana baina yao na matokeo yake juu ya uhusiano wa Lebanon na ndugu zao wa nchi za Kiarabu.Lebanon ilipatwa na mshtuko kutokana na hatua ya ghafla ya kujiuzulu kongozi huyo mnamo tarehe 4 Novemba akiwa Saudi Arabia na baadaye nchi hiyo iliyumba kutokana na Hariri kuendelea kubakia nchini Saudi Arabia muda mrefu baadaye.

Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud na waziri mkuu wa Lebanon Saad al-Hariri mjini Riadh (Reuters/Saudi Press Agency)

Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri na mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud

Kujiuzulu kwake kulionekana kama ni sababu ya kuuchochea mvutano kati ya mahasimu wakubwa na wababe wa wa muda mrefu wa eneo hilo, Saudi Arabia na Iran, hatua ambayo ilisababisha kuongezeka kwa hofu kwamba Lebanon ingekwama kutokana na mvutano huo wa kikanda. Wachambuzi wa mambo wanasema hatua ya leo ya Hariri kulifuta tamko lake la awali la kujiuzulu siku moja tu baada ya kurejea Lebanon ni kama kuitia aibu Saudi Arabia ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kuwa ndiyo iliyochochea kiongozi huyo kujiuzulu.

Katika maneno yake yaliyoashiria mapatano baada ya kutoka kwenye makaazi ya Rais Aoun, Hariri alisema anayaweka maslahi ya Lebanon kwanza kabla ya kitu chochote kile, huku akitarajia mahusiano mazuri baina ya vyama vyote vya kisiasa kwa ajili ya kuyapa nguvu matumaini ya Lebanon. Siku ya Jumatano Waziri Mkuu huyo alishiriki katika sherehe za uhuru wa Lebanon ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki katika hafla ya kitaifa tangu alipotangaza kujiuzulu.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com