Lavrov : Ukraine yakiuka makubaliano ya Geneva | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Lavrov : Ukraine yakiuka makubaliano ya Geneva

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov Jumatatu (21.04.2014) ameishutumu serikali ya Ukraine kwa kukiuka makubaliano ya kimataifa yaliofikiwa wiki iliopita kwa lengo la kuuzima mzozo wa Ukraine.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov akizungumza na waandishi wa habari Moscow.(21.04.2014)

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov akizungumza na waandishi wa habari Moscow.(21.04.2014)

Lavrov amesema katika mkutano na waandishi wa habari ulioonyeshwa na televisheni mjini Moscow "Makubaliano ya Geneva sio tu hayatimilizwi, lakini hatua zinachukuliwa hususan na wale walionyakua madaraka mjini Kiev ambazo zinakiuka kwa kiwango kikubwa makubaliano yaliofikiwa Geneva"

Alikuwa anazungumza baada ya kutolewa kwa onyo kutoka serikali ya Marekani kwamba wakati unayoyoma kutekeleza makubaliano hayo yaliofikiwa Geneva Alhamisi iliopita kati ya Urusi,Ukraine,Marekani na Umoja wa Ulaya.

Rais Barack Obama wa Marekani alikuwa ameionya Urusi kwamba itakabiliwa na vikwazo vya ziada iwapo hakuna hatua za maendeleo zitakazofikiwa katika siku chache zijazo.

Lakini Lavrov amepuuza hatari kwa Urusi kutumbukia kwenye hali ya kuzidi kutengwa kimataifa.Amesema majaribio ya kuitenga Urusi hayana mustakbali kwa sababu ni jambo lisilowezekana kuitenga Urusi duniani.

Wanaharakati bado kusamehewa

Wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika kituo cha ukaguzi karibu na mji Izium mashariki ya Ukraiane.(21.04.2014)

Wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika kituo cha ukaguzi karibu na mji Izium mashariki ya Ukraiane.(21.04.2014)

Ameongeza kusema kwamba viongozi wa serikali walioko katika mji mkuu wa Ukraine Kiev, hawakutoa msamaha kwa waandamanaji waliotiwa mbaroni kama vile inavyotakiwa na makubaliano ya Geneva.Lavrov amesema baada ya kuwaachilia wale ambao tayari wako mbaroni hasa gavana wa Donestsk,Pavel Gulbarev serikali ya Ukraine imekuwa kiendelea kuwakamata viongozi wa kisiasa kutoka kusini-mashariki ya Ukraine.

Pia amesema kwamba wito unaotolewa na wabunge wa Ukraine kuitunza kambi ya waandamanaji ilioko katika uwanja mkuu wa uhuru katika mji mkuu wa Kiev ambayo inajulikana kwa jina la Maidan ni "jambo lisilokubalika kabisa" akisema kwamba "hata kwa sheria ya Ukraine mambo hayo hayawezi kufanyika."

Amekiri kuhusu malalamiko ya serikali ya Ukraine kwamba makundi yanayoiunga mkono Urusi hayatimizi wajibu wao katika makubalinao ya Geneva, lakini ameishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kutochukuwa hatua ya kukomesha mzozo huo.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Urusi amesema wanalalamika kuhusu majimbo ya kusini-mashariki kwa kutoyaachia majengo wanayoyakalia na kuondowa vikwazo vya barabarani ,lakini serikali haichukuwi hatua yoyote ile, hawakunyanyuwa mkono kushughulikia sababu ambazo ndio msingi wa mzozo huo mkubwa wa Ukraine uliopo hivi sasa.

Makubaliano ya Geneva yatetereka

Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden akiwasili Kiev. (21.04.2014)

Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden akiwasili Kiev. (21.04.2014)

Makubaliano yaliofikiwa Geneva wiki iliopita ya kuepusha kutanukwa kwa mzozo huo wa Ukraine yametetereka wakati wiki mpya ikianza huku kukiwa hakuna dalili kwa wanamgambo wenye kuiunga mkono Urusi kuyasalimisha majengo ya serikali ambayo wameyanyakuwa.

Serikali ya Marekani imesema itaiwajibisha serikali ya Urusi na kuiwekea vikwazo vipya vya kiuchumi iwapo wanaharakati hao wanaotaka kujitenga hawatoondoka kwenye majengo ya serikali wanayoyakalia kwa mabavu katika sehemu kubwa ya mashariki ya Ukraine tokea wiki mbili zilizopita.Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden leo amewasili katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev.

Serikali ya Ukraine na Urusi zimekuwa zikishutumiana kutokana na mashambulio ya risasi yaliosababisha maafa asubuhi ya Jumapili ya Pasaka,ambapo takriban watu watatu waliuwawa katika kituo cha ukaguzi kinachosimamiwa na wanaharakati wanaotaka kujitenga wenye silaha.Urusi na wanaharakati hao wanaotaka kujitenga wamewashutumu wanaharakati wa sera za utaifa wa Ukraine kwa kukishambulia kituo hicho cha ukaguzi, wakati serikali ya Ukraine inasema Urusi ilianzisha uchokozi huo.

Wanaharakati kupatiwa paspoti za Urusi

Wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mji wa Slovyansk mashariki ya Ukraine.

Wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mji wa Slovyansk mashariki ya Ukraine.

Katika hatua yake ya karibuni ambayo yumkini ikaonekana na mataifa ya magharibi kuwa tishio zaidi kuelekea katika hali ilioko zamani ya Vita Baridi,Rais Vladimir Putin wa Urusi leo amesaini sheria ambayo inafanya iwe rahisi kwa watu wenye nasaba ya Kirusi kutoka jimbo hilo la zamani la Muungano wa Kisovieti kujipatia uraia wa Urusi.

Wanaharakati wanaotaka kujitenga wamejitangazia uhuru kwa "Jamhuri ya Watu wa Donetsk" katika jimbo kubwa kabisa lilioko mashariki ya Ukraine na kujitangazia nyadhifa za serikali katika miji mikubwa na midogo,kuweka vituo vya ukaguzi na kupeperusha bendera za Urusi karibu na majengo ya serikali.

Serikali ya Ukraine imetangaza "Suluhu ya Pasaka" juu ya kwamba haifahamiki kabisa iwapo inaweza kutumia nguvu za kweli iwapo itajaribu.Jeshi la nchi hiyo lina silaha chache, halikuwahi kufanyiwa majaribio na halikupatiwa mafunzo kwa ajili ya operesheni za ndani ya nchi wakati serikali yenye makao yake huko Kiev ikiutilia mashaka uaminifu wa polisi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/Reuters

Mhariri : Mtullya Abdu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com