1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lars Bender nje ya kikosi cha Ujerumani

23 Mei 2014

Kiungo wa Bayer Leverkusen Lars Bender amepata jeraha la paja ambalo limemnyima tikiti ya kucheza dimba la Kombe la Dunia nchini Brazil. Kocha Joachim Löw hatomwita kikosini mchezaji mpya kuchukua nafasi yake.

https://p.dw.com/p/1C5Bu
Fußballspieler Lars Bender
Picha: picture-alliance/dpa

Wasiwasi wa majeruhi katika kikosi cha Ujerumani yameongezeka wakati kiungo Lars Bender alipata jeraha ambalo litamnyima fursa ya kucheza dimba la Kombe la Dunia nchini Brazil mwezi ujao. Taarifa kutoka kwa kikosi cha Ujerumani kinachoendelea na mazoezi nchini Italia imesema kiungo huyo wa Bayer Leverkusen alilazimika kujiondoa kutoka katika kikosi cha mwanzo cha wachezaji 27.

Kocha Löw amesema “Inasikitisha sana kwa kila mtu wakati mchezaji anapolazimika kujiondoa kikosini kwa sababu ya jeraha wakati kinyang'anyiro kikikaribia”. Bender ameichezea mechi nyingi klabu ya Leverkusen msimu huu na pia ana uwezo wa kucheza kama beki ya kulia, kwa sababu amewahi kucheza katika nafasi hiyo katika timu ya taifa.

“ninamhurumia sana Lars. Najua kuwa alitaka sana kuwa nchini Brazil. Kwa misingi ya nidhamu, na uwezo wa kispoti, yeye ni kielelezo”. Ameongeza Löw. Ujerumani kwa sasa wako katika jimbo la Tyrol Kusini, kwa ajili ya kambi ya mazoezi kabla ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon mnamo Juni mosi. Kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 kitachaguliwa mnamo Juni 2. Washindi hao mara tatu wa Kombe la Dunia wamepangwa katika kundi G pamoja na Ureno, Ghana na Marekani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef