Larijani aitetea Iran | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Larijani aitetea Iran

Mpatanishi wa Iran katika mzozo wa nyuklia, Ali Larijani, aliitetea nchi yake kwenye mkutano wa usalama uliofanyika mjini Munich hapa Ujerumanimwishoni mwa juma. Wakati huo huo waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, aliutolea mwito mkutano huo uheshimu ahadi zilizotolewa kwa Afghanistan.

Mpatinishi wa Iran katika mzozo wa nyuklia Ali Larijani

Mpatinishi wa Iran katika mzozo wa nyuklia Ali Larijani

Katika mkutano kuhusu usalama uliomalizika mwishoni mwa juma mjini Munich hapa Ujerumani, mpatinishi wa Iran katika mzozo wa nyuklia, Ali Larijani, alisema Iran inataka kuendeleza mpango wake wa nyuklia kwa matumizi ya amani, licha ya kitisho cha kuwekewa vikwazo iwapo haitasitisha urutubishaji wa madini ya uranium katika kipindi cha siku kumi zijazo. Larijani alisisitiza kwamba nchi yake inapinga umilikaji wa silaha za kinyuklia.

Mwanzoni mwa mkutano wa mjini Munich, kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, aliitaka Iran iachane na mpango wake wa nyuklia.

Larijani aliahidi kwamba Iran iko tayari kushirikiana na mataifa mengine kuutanzua mzozo wake wa nyuklia.

´Tumetangaza wazi kwamba katika sera yetu kuhusu usalama hakuna nafasi kwa silaha za kinyuklia na kemikali. Na tunajua pia kwamba tutakapotengeza silaha za kinyuklia, madola kuu kwa upande wao zitatengeza silaha hizo katika mataifa jirani, jambo litakalosababisha mashindano ya umilikaji wa silaha katika eneo zima. Ndio maana tunapinga. Pamoja na hayo tuna wasiwasi kwamba magaidi wanaweza kufanikiwa kumiliki silaha za aina hiyo.´

Mapendekezo yanaweza kuwasilishwa kwa Iran bila kuiwekea mbinyo ifanye nini hasa, alisema Larijani mjini Munich. Kushiriki kwa Larijani katika mkutano wa Munich ni ishara ya matumaini hasa ikizingatiwa kwamba vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran huenda vikaanza kutekelezwa ifikapo tarehe 20 mwezi huu.

Kufikia mwisho wa mkutano wa Munich hatua ya rais wa Urusi Vladamir Putin kuikosoa Marekani na shirika la NATO ilibakia mada muhimu. Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates aliutumia mkutano wa Munich kutoa jibu lake.

´Urusi ni mshirika wetu, lakini tunashangazwa pia na maamuzi kadhaa yanayohatarisha utengemano wa kimataifa. Kwa mfano usafirishaji wa silaha na jaribio la kutumia nishati kama silaha ya kisiasa. Urusi haihitaji kuogopa kabla kuwa na demokrasia ndani ya mipaka yake.´

Katika hotuba yake waziri Gates alisema Marekani haitaki vita vipya vya baridi. Mkutano wa mjini Munich ulihudhuriwa na mawaziri wa mashauri ya kigeni na mawaziri wa ulinzi wa shirika la NATO. Akizungumzia Afghanistan waziri Gates alisema ipo haja ya kuzitimiza ahadi zilizotolewa kwa kutumia fedha na wanajeshi.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, akizungumzia kuhusu kuipa nafasi amani nchini Afghanistan, hakuikosoa tu Marekani bali pia Wajerumani kuhusu matumizi ya harakati za kijeshi.

´Wajerumani wengi wanang´ang´ana na uelewa kwamba jukumu la kimataifa linaweza kujumulisha kupeleka jeshi ikilazimika. Kinyume cha hayo, wengi nchini Marekani wanajifunza kwamba demokrasia haiwezi kulazimishwa kupitia harakati za kijeshi.´

Waziri Steinmeier alilikosoa shirika la NATO kwa kutoshirikiana kikamilifu kulinda usalama wa viumbe duniani. Aliuliza kama uhaba wa maji, kuenea kwa jangwa au teknolojia ya kutengeneza nishati ni matatizo yanayoweza kujadiliwa kwenye mikutano ya shirika la NATO.

 • Tarehe 12.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHKP
 • Tarehe 12.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHKP

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com