1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lakhdar Brahimi asema anahofu ya majukumu yake

MjahidA3 Septemba 2012

Mjumbe aliyeteuliwa kutatua mzozo wa Syria Lakhdar Brahimi, amesema Juhudi za kidiplomasia za kujaribu kuumaliza mzozo wa Syria zinakaribia kushindikana na hakuna hatua za kutosha zinazochukuliwa kukomesha vita

https://p.dw.com/p/162We
Mjumbe aliyeteuliwa kutatua mzozo wa Syria Lakhdar Brahimi
Mjumbe aliyeteuliwa kutatua mzozo wa Syria Lakhdar BrahimiPicha: Reuters

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za kiarabu katika kuutatua mzozo wa Syria Lakhdar Brahimi, amesema hakuna hatua za kutosha zinazochukuliwa kuhakikisha ghasia nchini Syria zinasimamishwa, na hilo ni jambo ambalo linampa uzito katika kazi yake.

Sasa Brahimi amesema anahofu ya majukumu aliyopewa sababu bado watu wanaendelea kuangamia nchini humo na haoni juhudi zaidi katika kukomesha mapigano.Kauli ya mjumbe huyo imetolewa wakati akizungumza na shirika la habari la Uingereza BBC.

"Bila shaka hii ni kazi ngumu sana, ninahofu ya uzito wa majukumu yangu, tayari watu wanasema kwamba, watu Syria wanakufa unafanya nini kusaidia? kwa kweli hatufanyi mengi na hilo pekee ni suala zito. Nimegundua umuhimu na ugumu wa majukumu haya" Alisema Brahimi.

Lakhdar Brahimi, amesema anahisi ni kama amesimama katika kizingiti bila ya suluhu yoyote. Brahimi ambaye ni mwanadiplomasia kutoka Algeria alichukuwa nafasi ya Kofi Annan kushughulikia mzozo wa Syria baada ya Annan kujiondoa mwezi uliopita. Annan alijiuzulu baada ya kulalamikia hatua za baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kujaribu kukwamisha juhudi za kupatikana amani nchini Syria.

Mashambulizi zaidi Syria
Mashambulizi zaidi SyriaPicha: dapd

Tangu kuanza kwa vuguvugu la maandamano nchini Syria, kutaka kumuondoa madarakani rais Bashar Al Assad miezi 17 iliopita, zaidi ya watu 20,000 wameuwawa kufuatia mapambano makali kati ya waandamanaji na jeshi la serikali ya nchi hiyo linalotaka kuwakandamiza waandamanaji.

Huku hayo yakiarifiwa ndege ya kivita ya Syria ilishambulia jengo moja kaskazini mwa mji wa waasi wa Al-Bab na kusababisha vifo vya watu 18. Hii ni kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu nchini humo. Akizungumza na shirika la habari la AFP Mkurugenzi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman, amesema kati ya waliouwawa ni wanaume 10, wanawake 6 na watoto wawili.

Shirika hilo limeyataja mauaji yaliofanywa mwezi wa Agosti kuwa mauaji mabaya zaidi kufanyika katika mwezi huo ambapo watu takriban 5,440 waliuwawa.

Mataifa ya Ghuba yalaani mapigano Syria

Kwa upande mwengine mataifa ya Ghuba yameilaumu Syria kwa kutumia silaha nzito nzito dhidi ya waandamanaji. Mataifa hayo kwa sasa yamesisitiza amani katika juhudi za kuwepo kipindi cha mpito cha kugawana madaraka nchini humo.

Wanachama wa Mataifa ya Ghuba
Wanachama wa Mataifa ya GhubaPicha: picture-alliance/dpa

Mataifa sita wanachama wa nchi za ghuba ikiwemo Saudi Arabia, Bahrain, Umoja wa falme za kiarabu, Oman, Qatar na Kuwait pia wamehimiza jamii ya kimataifa kuchukua jukumu zaidi na kutoa mikakati ya kulinda raia nchini Syria.

Hata hivyo Jihad Makdissi, msemaji katika serikali ya Bashar Al Assad amesema Lakhdar Brahimi, mjumbe aliyeteuliwa kutatua mzozo wa Syria baada ya kujiuzulu kwa Annan atafanya ziara yake mjini Damascus hivi karibuni.

Mwandishi Amina Abubakar

Mhariri Yusuf Saumu