1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kyrgyzstan yatarajiwa kuunda serikali ya mseto

11 Oktoba 2010

Chama kinachoungwa mkono na Urusi cha Ar-Namys kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Felix Kulov kimejitangazia ushindi katika Uchaguzi wa Bunge, lakini hali inaonesha hakiwezi peke yake kuunda Serikali

https://p.dw.com/p/Pb4W
Asilimia 56.59 ya wapiga kura walishiriki katika uchaguzi huo
Asilimia 56.59 ya wapiga kura walishiriki katika uchaguzi huoPicha: AP

Taifa hilo linaonekana litaweza kuunda serikali ya muungano kutokana na kinyang’anyiro kati ya vyama vikuu vitano, taswira ambayo ni tofauti katika kanda hiyo ambayo inasifika kwa kuwa na marais wenye udhibiti na mabunge hafifu.

Viongozi wamekisifu kiwango cha asilimia 56.59 ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi huo na waliopuuza onyo kwamba uchaguzi huo ungegubikwa na machafuko mapya ya kisiasa na kikabila kama yaliyotokea mwaka huu.

Kiongozi wa serikali ya mpito wa Kyrgyzstan, Rosa Otunbayeva
Kiongozi wa serikali ya mpito wa Kyrgyzstan, Rosa OtunbayevaPicha: AP

Rais Roza Otunbayeva ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kuleta mfumo mpya wa kisiasa, baada ya kupiga kura yake, alisema ni siku ya kihistoria kwa Jamhuri ya Kyrgyzstan ambapo raia watachagua hatima ya mustakabali wao.

Kyrgyzstan iliunda bunge la kwanza la kidemokrasia katika kanda ya bara Asia ya kati, katika kura ya maoni mapema mwaka huu baada ya mapinduzi ya umwagaji damu mwezi Aprili uliomwondoa madrakani rais Kurmanbek Bakiyev na kusababisha ghasia za kikabila mwezi Juni.

Kulingana na matokeo yaliyochapishwa kwenye tovuti ya habari ya Centrasia, iliyowahoji zaidi ya wapiga kura 1,300, chama cha Ar-Namys kitaweza kuibuka na ushindi wa asilimia 22.1 katikia uchaguzi huo, kikifuatwa na chama cha Social Democratic kinachounga mkono serikali, kwa asilimia 20.7.

Takwimu ya tume ya uchaguzi nchini humo, inaonyesha chama cha Ata-Zhurt kinaongoza kwa asilimia 8.9 ya kura kutokana na hesabu ya nusu ya kura iliyopigwa. Chama cha Social Democratic kina asilimia 8.4, chama cha Ar-Namys kina asilimia 6.9 na hadi kufikia sasa chama cha Republic kiko katika nafasi ya nne kwa asilimia 6.85.

Ikiwa mwelekeo huo utaendelea, vyama vitano vitaingia katika bunge linalojulikana kama 'Zhogorku Kenesh' ambapo ushindi wa asilimia tano ya kura unahitajika ili chama kiwe na viti bungeni.

Mwanasiasa Felix Kulov aliyepokelewa na rais wa Urusi Dmitry Medvedev kabla ya uchaguzi huo alifanya kampeni yake kwa misingi ya kufuata sheria na aliapa kurejesha uongozi wa mfumo wa urais unaopigiwa upatu na Urusi.

Kyrgyzstan ni taifa la kipekee duniani ambalo lina makambi mawili ya wanajeshi wa Marekani na Urusi na lipo katika eneo muhimu linalopakana na China na liko karibu na Afghanistan, hivyo kuwa kambi muhimu kwa wanajeshi wa Marekani.

Machafuko ya mwezi Juni kati ya makabila ya Wa-Uzbeki walio wachache na Wa-Kyrgizi yalisababisha vifo vya kati ya raia 400 na 2000 katika mji wa Osh ulioko kusini mwa nchi hiyo.

Mwandishi: Peter Moss/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed