Kwanini Obama amemchagua Hillary Clinton ? | Magazetini | DW | 03.12.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Kwanini Obama amemchagua Hillary Clinton ?

Wahariri wachambua mada mbali mbali tangu nchini hata nje.

Obama akimlahki Clinton.

Obama akimlahki Clinton.

Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo umezungumzia mada mbali mbali-kuanzia rais Bush na vita vyake nchini Irak,Kwanini rais mteule Barack Obama amemteua mpinzani wake Hilary Clinton waziri wa nje,hodi-hodi za Georgia kutaka uanachama katika shirika la ulinzi la Nato,mzozo wa kisiasa nchini Thailand hadi hatua zinazofaa kuufufua uchumi humu nchini: Gazeti la Dithmarscher Landeszeitung juu ya vita vya George Bush nchini Irak akikaribia kuacha madaraka laandika:

"Nadra kutokea kwa Marekani kutamani Rais wao aondoke madarakani kama wanavyotamani kwa George Bush.Maoni yao juu ya kipindi chake cha utawala hata kwa wafuasi wengi wa chama chake cha Republikan si ya kupendeza. Na kwavile sasa hana hata siku 50 za kubakia madarakani na ni kama rais jina tu,Bush anajaribu kufuta madhambi yake na kukuza kidogo heba yake .

Katika mahojiano ameungama kufanya makosa katika vita vya Irak.Lakini hii haina maana kuwa Bush anajitwika dhamana ya kuuwawa kwa maalfu ya wanajeshi na raia. Ametaja tu taarifa zisizo sahihi alizopewa na Idara za ujasusi juu ya silaha za kuhilikisha umma nchini Irak...."

Ama gazeti la Ostthuringer Zeitung kutoka Gera linachambua azma ya Obama kumteua mpinzani wake Hillary Clinton waziri wa nje katika serikali yake.Laandika:

"Azma ya Obama ni kumfunga pingu za kisiasa Hillary Clinton ili aweze kumdhibiti.Asingefanya hivyo angekabiliwa na upepo mkali huko Kapitol.

Pia amefikiria hapo uwezo wake,kwani anaelewa mnamo miaka 80 iliopita hakuna rais alieingia Ikulu bila maarifa makubwa kama yeye.Kwahivyo, kwanini asitegemee maarifa ya Clinton na hata ya waziri wa ulinzi Gates wa utawala wa George Bush .Obama anaelewa kasoro ya maarifa ndipo ulipo udhaifu wake mkubwa na kwavile anaelewa hivyo, ndipo nguvu zake zilipo."

Kuhusu hodi hodi za Georgia kujiunga na shirika la ulinzi la magharibi (NATO) gazeti la Nuremberger Nachrichten laandika:

"Rais wa Georgia Saakaschwili yamkini ni rafiki wa chanda na pete wa Georrge Bush,lakini huo sio msingi wa kupewa uwanachama wa NATO. Mwanasiasa huyu amekiuka kanuni za kimsingi za demokrasia ya nchi za magharibi inayosema: Kwa kadiri juhudi za kibalozi hazikushindwa,pasitumiwe nguvu.

Nchi ilio na uongozi kama huo, haina lake katika NATO.Kwani, Georgia si swali la kuletas usalama ,bali ni hatari kwa usalama."

Katika mjadala jinsi gani kuufufua uchumi kufuatia mzozo wa fedha uliozuka,gazeti la Norwest-Zeitung laandika:

"Sauti zinazidi kupazwa zikidai fedha zitolewe kuwatia jeki raia kutumia.Kima cha kati ya Euro 250 hadi 500 kinazungumzwa. Bila shaka hizo ni fedha nyingi ambazo wengi wangehitaji kutumia.Lakini kugawa fedha hizo hakutasaidia sana kuuzima moto.Kwahivyo, serikali ya Ujerumani inabidi mwakani 2009 kupunguza kodi na hasa zile za mapato."