Kwa nini bei za chakula zimepanda? | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.04.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kwa nini bei za chakula zimepanda?

Kupanda kwa bei za vyakula vya kawaida kumezusha mjadala. Mkuu wa kitovu cha kiuchumi cha Deutsche Welle, Bw. Karl Zawadzky, amechuguza kwa nini bei za vyakula zimepanda hivi na suluhusiho ni lipi.

Machafuko nchini Haiti baada ya maandamano dhidi ya bei kubwa za chakula

Machafuko nchini Haiti baada ya maandamano dhidi ya bei kubwa za chakula

Wakati wakaazi wa nchi tajiri wana wasiwasi kuhusu bei kubwa za mafuta, watu katika nchi maskini tayari hawawezi kujaza matumbo yao. Suala la mafuta ni moja kati ya vyanzo vilivyosababisha ongezeko la bei za vyakula, kwa sababu vyakula vinatumiwa kutengeza mafuta. Lakini kuna vyanzo vingine. Kwa mfano ongezeko la idadi ya binadamu duniani. Kila mwaka idadi hii inakua kwa watu millioni 80 ambao wanahitaji kulishwa. Kulingana na makadirio, idadi ya watu duniani itakua kwa asilimia 50 hadi mwaka 2050, wengi wao watazaliwa katika nchi zinazoendelea ambapo tayari leo mamillioni ya watu hawana chakula cha kutosha, na maelfu wanakufa na njaa kila siku.


Wakati huo huo, ardhi yetu ina rutuba ya kutosha kuwalisha watu wengi kuliko wanaoishi hii leo. Kwa hivyo, utapiamlo, njaa na vifo vya njaa si lazima. Tayari miaka 20 iliyopita, shirika ka vyakula vya Umoja wa Mataifa limetambua kwamba "tatizo si uhaba wa chakula bali uhaba wa nia ya kisiasa." Maneno haya yana uzito hata leo. Kati ya watu watano ulimwenguni, mmoja hana fedha zaidi ya thamani Dola moja kwa siku, ndiyo yeye ambaye atalala na njaa au kufa kwa njaa. Pale lakini ambapo watu wanazidi kupata ajira na kumudu chakula, njaa inapungua. Basi, njia muhimu zaidi kutatua tatizo la njaa ni kutoa ajira na kuwapatia watu mapato. Lakini tena, hilo peke yake halitoshi.


Mzozo huu wa chakula ambao ulisababisha maandamano na ghasia katika nchi kadhaa unatokana pia na mfumuko wa bei duniani kote pamoja na kubadilishwa njia za biashara. Hususan katika nchi zinazoendelea haraka kama China na India, mahitaji ya chakula yanatimizwa kwa kuagiza kiasi kikubwa cha chakula. Kwa sababu hiyo na nyingine, bei za vyakula kama mahindi na mchele zimepanda kupita kiasi. Na bado zinatarajiwa kuongeza zaidi, kwa sababu wafanyakazi wa nchi zinazoendelea haraka wanataka kula chakula bora kama nyama. Kwa hivyo, sehemu kubwa ya ngano itatumika kulishia wanyama badala ya kutengeneza unga na kadhalika. Wanaoathirika ni maskini. Kimsingi basi tunaweza kusema, kuongezeka kwa utajiri katika sehemu moja ya dunia kunasababisha kuongezeka kwa umaskini sehemu nyingine.


Hata hivyo, tusisahau kwamba ongezeko hilo la bei linaweza kuzinufaisha nchi maskini. Sharti lake ni kwamba nchi za kiviwanda zikubali kufuta ruzuku kwa wakulima wao na kufungua masoko yao kwa bidhaa kutoka nchi zinazoendelea. Kwani katika uzalishaji, bidhaa hizo kutoka nchi maskini zinaweza kushindana na soko la kimataifa, lakini zinazuiliwa kupitia ushuru wa forodha na ruzuku. Wakati huu ni mwafaka kabisa kumaliza uovu huu. Kama nchi maskini zitaweza kuuza mazao yao katika nchi tajiri, zitaweza pia kuongeza nafasi za ajira na mapato kwa wananchi wao. Wenye njaa na maskini wa dunia hii wanahitaji misaada ya chakula, lakini wanachokihitaji zaidi ni ajira na biashara sawa ili kujikomboa kutoka hali hii.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com