Kutengwa Qatar na mashambulizi ya London Magazetini | Magazetini | DW | 07.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Kutengwa Qatar na mashambulizi ya London Magazetini

Uamuzi wa kutengwa Qatar, shambulio la kigaidi la mjini London na suala kama lingeweza kuepukwa na lawama dhidi ya katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa magazetini

Tunaanza na mzozo wa Ghuba. Wahariri wanakubaliana chanzo halisi ni chengine kabisa . Mhariri wa gazeti la mjini Lüneburg,"Landeszeitung" anaandika: "Kutengwa Qatar hakuhusiani hata kidogo na ugaidi, chanzo chake hasa ni kiu cha kujipatia madaraka Saud Arabia.Tuhuma kwamba Qatar inayasaidia makundi ya kigaidi pengine si za uwongo. Lakini kama kuna  yeyote wa kukaa kimya basi ni Saud Arabia. Kwasababu kwa miaka sasa  Saud Arabia imekuwa katika dhana ya kuwaunga mkono magaidi. Ukweli ni kwamba nchi hiyo ya kifalme inataka kuunda ushirikiano pamoja na nchi nyengine jirani zinazofuata madhehebu ya sunni ili kuuvunja nguvu ushawishi mkubwa wa Teheran. Zaidi ya hayo mfalme Salman wa Saud Arabia anahofia uasi wa jamii ya wachache ya shia katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo-kunakokutikana shehena kubwa zaidi ya mafuta. Salman hafichi, anataka nchi yake yenye nguvu kubwa za kiuchumi katika ulimwengu wa kiarabu iwe pia nguvu kubwa zaidi kisiasa. Lakini kuitenga Qatar ni hatua ya mwanzo tu inayoweza kusababisha vurugu katika eneo lote hilo .

Majuto mjukuu wanasema waengereza

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anakosolewa kwa kuamua alipokuwa waziri wa mambo ya ndani kupunguza idadi ya polisi au Bobby kama wanavyoitwa nchini Uingereza. Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung linachambua lawama hizo na kuandika: "Majuto mjukuu. Lakini katika kadhia ya mashambulio ya hivi karibuni mjini London, watu wangeweza tangu mapema kujiepushia majuto-wangeweza kuwa werevu zaidi kuliko vile alivyokuwa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May. Alipokuwa waziri wa mambo ya ndani, yeye ndie aliyeamuru zifutwe nafasi 20.000 za kazi za askari polisi au Bobbys. Nafasi hizo ndizo zile zilizopungua ili kuwawezesha polisi kutekeleza ipasavyo shughuli zao katika jamii. Bobbys wamekuwa wakiangaliwa kua  "wenye bidii" hata kabla ya neno hilo kuenea katika sehemu ya bara ya Ulaya."

Stoltenberg anaonyesha kazidiwa

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na mzozo wa Uturuki na Ujerumani, nchi mbili wanachama wa jumuia ya kujihami ya NATO na jinsi katibu mkuu wa jumuia hiyo Jens Stoltenberg anavyouangalia mzozo huo. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linahisi: "Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO haonyeshi kuwa muwfak kwa jumuia hiyo kwa sasa. Kwanza Stoltenberg alionekana kuwa msikilizaji mtiifu wa rais mpya Marekani na kumwachia Donald Trump kufika hadi ya kuwakaripia hadharani wanachama wa NATO eti hawalipi michango yao . Baadae akayataja malumbano kati ya Uturuki na Ujerumani kuhusu kituo cha jeshi la wanaanga cha Incirlik kuwa ni mzozo wa ndani kati ya Berlin na Ankara na haumhusu mtu yeyote mwengine. Mnamo wakati kama huu jumuia ya NATO ingestahiki kuwa na kiongozi mkakamavu, anaetambua madhara jumla yanayoweza kusbabishwa na mzozo kama huu kati ya washirika wawili wa NATO. Badala yake Stoltenberg ananyamaza kimya anafanya kana kwamba hayajamhusu.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com