Kutekwa nyara watalii nchini Misri | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kutekwa nyara watalii nchini Misri

Dola milioni sita zinahitajika kuwakomboa mahabusi wa kitalii

default

Jangwa linalotanda baina ya Misri na Sudan ambako watalii wa Kijerumani wanaripotiwa kutekwa nyara

Maafisa wa Kijerumani wanashauriana na watu waliowateka nyara watalii 11 na raia wanane wa Misri ambao walipotea ijumaa iliopita katika jangwa lililoko Kusini mwa Misri pale walipokuwa wakifanya safari ya kitalii. Duru kutoka wizara ya utalii ya Misri zilisema leo kwamba mashauriano yanaendelea ili waachwe huru Wazungu hao 11, wakiwemo Wajerumani watano, Wataliana watano na Mrumania mmoja, pamoja na Wamisri wanane waliokuwa wanauongoza msafara huo.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani imeunda kikundi cha kuushughulikia mkasa huo, punde pale habari za kutekwa nyara watu hao zilipozagaa jana alasiri. Msemaji wa wizara hiyo alisema bado wanachukulia kwamba kisa hicho ni cha utekaji nyara, na wako mbioni sana kuutanzuwa mzozo huo. Lakini alikataa kusema kama mashauriano hayo yanafanyika na watekaji nyara au kama fedha za fidia zitalipwa. Msemaji katika wizara ya utalii ya Misri alisema serekali yao ilikuwa inayafuatiliza mashauriano hayo, bila ya kutoa maelezo zaidi. Misri imekanusha kwamba inafanya mashauriano moja kwa moja na watekaji nyara hao, huku waziri wake wa utalii, Zuhair Garana, akisema Ujerumani inafanya mawasiliano na watekaji nyara. Aliongeza kusema hivi:

" Mmoja kati ya watu waliotekwa nyara, kwa hakika, ana mawasiliano na mkewe ambaye ni Mjerumani. Mtu huyo ni Mmisri ambaye anaumiliki wakala wa misafara wa Misri. Aliwasiliana na mkewe na alimuarifu kwamba wametekwa nyara na kwamba kuna fidia ya fedha inayotakiwa serekali ya Ujerumani ilipe."

Inasemakana watekaji nyara hao wanataka walipwe hadi dola za Kimarekani milioni sita taslimu.

Ripoti zisizohakikishwa zinasema watekaji nyara wamewatishia kuwauwa mahabusu wao pindi kutakuweko ujiingizaji wa kijeshi kutaka waachiliwe huru watalii hao.

Watu hao 19 walitekwa nyara ijumaa iliopita walipokuwa wanalitembelea eneo la Gilf Kebir, eneo la utalii lililoko katika jangwa, Magharibi ya Misri, ambalo ni maarufu kwa michoro ya kale ilioko katika mapango ya majabali. Habari za utekaji nyara huo zilipatikana tu jumatatu pale mmoja kati ya waongozaji wa misafara kutokea Misri alipompigia simu mkewe wa Kijerumani kumpa habari hiyo. Mwezi Januari mwaka huu, kikundi cha Wajerumani kilishambuliwa na kuibiwa katika eneo hilo hilo. Waliachwa jangwani wakiwa hawana kitu isipokuwa simu yao ya Satellite. Haijulikani nani walifanya shambulio hilo.

Wasifa wa watekaji nyara hawa wa sasa haujahakikishwa, japokuwa wizara ya mambo ya kigeni ya Misri ilisema ni maharamia na sio magaidi. Na Televisheni ya al-Jazeera, ikiwanukulu maafisa wa Kimisri wasiotajwa, ilisema leo kwamba watekaji nyara hao ni majangili wa kutokea Chad.

Pia Misri imetuma kikundi cha majasusi hadi eneo hilo la Kusini ambako watu hao waliotekwa nyara wanaaminiwa wako. Majasusi hao wanashirikiana na maafisa wa usalama wa Sudan ili kuhakikisha watu waliotekwa nyara wanaachwa huru. Waziri wa utalii wa Misri Zoheir Garana, aliiambia televisheni ya nchi yake kwamba huenda watekaji nyara hao ni Wa-Sudan, lakini duru za usalama jana zilisema wanaweza kuwa ni raia wa nchi jirani ya Chad ambako waasi wa Sudan na wa Chad wanafanya harakati zao. Lakini afisa wa wizara ya mambo ya kigeni ya Sudan alisema haiwezekani kwamba mahabusu hao wako Sudan kwa sababu ya usalama mipakani na kwamba kunakosekana mahala pa kujifichia katika maeneo hayo ya mbali.
 • Tarehe 24.09.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FOGy
 • Tarehe 24.09.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FOGy
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com