1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutawazwa Obama mtetezi rasmi

28 Agosti 2008

Uchambuzi wa wahariri umetuwama leo juu ya Obama na changamoto kati ya Russia na Magharibi juu ya georgia.

https://p.dw.com/p/F6M1

Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo, umetuwama zaidi juu ya kutawazwa jana kwa Barack Obama kama mtetezi rasmi wa Chama cha Democrat kwa urais wa Marekani.

Mada nyengine iliowashughulisha wahariri, ni mvutano kati ya kambi ya magharibi na Russia kuhusu Georgia.Ilikua zamu tena ya Ramadhan Ali kuzikagua safu hizo za wahariri akianza na SAARBRUCKER ZEITUNG-nalo laandika:►◄

"Hillary Clinton, ameonesha katika mkutano mkuu wa chama cha Democrat jana kuwa ni mwanasiasa aliekomaa kwa werevu.Hakufanya hivyo kwa kuwa ghafula ,amegundua mapenzi kwa Obama, bali kwa masilahi yake mwenyewe ya kisiasa kwa siku za usoni.Ndio maana amejitokeza wazi wazi na bila kigeugeu nyuma ya Obama kugombea urais.

Mtetezi huyu wa kiti cha urais alieshindwa chupuchupu alin*gamua angemtilia Obama kitumbua chake mchanga,basi nae angekuja kukiona cha mtemakuni....hujuma yake aliyoivurumisha dhidi ya John McCain,aliifanya kusudi kuwafuta machozi wafuasi wake.Kwa njia hii, Hillary Clinton amejijenga bila kubidi kumpigia magoti Obama."

Ama gazeti la Darmstądter Echo likiendeleza mada hii laandika:

" Yule aliekua na maoni kwamba huko Denver,sasa imeanza enzi ya Barack Obama ,huyo alikosea.Kwani, wageni wasioombwa na kinyume na wenyeji wao,walitamba katika jukwaa la Obama:Hotuba ya Bibi Clinton,iliupambamba zaidi mkutano huo uliohanikiza katika vyombo vya habari."

Likikamilishia mada hii kwa leo, gazeti la Munchner Merkur,

laonya:

"Ikiwa mwishoe, Obama hatafaulu kuchaguliwa rais,basi itatokana na akina Clinton.Licha ya kwamba Bibi Hillary na mumewe Clinton walimjenga jana Obama,wafuasi wao wengi kati ya milioni 18 wakimuangalia Obama kwa jicho la shaka shaka.

Na hasa wale wazungu wa tabaka la kati na kati ambao wanahofia hali zao za maisha zaweza zikazidi kuteremka.Hotuba nzuri mara hii haitoshi. Suluhisho ameligundua Obama kutoka Bill Clinton alietambua kwamba ufunguo ni kuboresha uchumi.Bila kuimarisha uchumi haitawezekana kufanikiwa."

Likutuchukua sasa katika mvutano kati ya Russia na kambi ya magharibi juu ya mzozo wa Georgia,gazeti la Aachener Zeitung laandika:

"Kwa mara ya kwanza tangu miaka 20,Moscow imefaulu kuitia hofu kambi ya magharibi.Na kabisa hii ndio ilikua shabaha yake hata ikiwa tangu rais Medwedew hata waziri wake mkuu Wladmir Putin,wadai hiyo si nia yao.

Russia inataka kupindukia nchi jirani kidogo ianze kuogopwa tena na imepania kutetea masilahi yake kwa nguvu zaidi.

Kwa jicho la Ujerumani kuonesha nia kama hiyo, Russia,haielewiki kabisa. Juu ya hivyo, wanasiasa wa madola makuu huwa hiyo ni tabia yao.

Tawala za kimabavu na madikteta huwa rahisi kwao kukanyaga haki za kimataifa.Hawajali kuwaheshimu wanaowapinga,uhuru wa magazeti na umma unaokosoa pamoja na malalamiko ya walimwengu.Kinyume chake:Vyombo vyao vya propaganda huvitumia kuona wanaungwamkono katika shabaha zao."