Kura ya maoni ya Katalonia Magazetini | Magazetini | DW | 02.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Kura ya maoni ya Katalonia Magazetini

Kura ya maoni iliyozusha machafuko katika jimbo la Uhispania la Katalonia, na juhudi za kuunda serikali ya muungano baada ya uchaguzi mkuu ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri magazetini

Kura ya maoni iliyozusha machafuko katika jimbo la Uhispania la Katalonia, juhudi za kuunda serikali ya muungano baada ya uchaguzi mkuu na miaka 27 ya muungano wa Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tunaanzia katika jimbo la kaskazini mashariki mwa Uhispania-Katalonia ambako wapiga kura zaidi ya milioni mbili kati ya wakaazi milioni saba na nusu wa jimbo hilo tajiri la Uhispania waliteremka vituoni jana katika zoezi la kura ya maoni linalozusha mabishano na ambalo hatima yake hakuna anaeweza kuikadiria. Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linaandika:

"Kwamba serikali kuu ya mjini Madrid haipendezewi hata kidogo na juhudi za kupigania uhuru wa jimbo hilo tajiri, ni jambo linaloeleweka. Lakini kisichoeleweka hata kidogo ni yale matumizi ya nguvu yaliyokithiri ya vikosi vya serikali ya waziri mkuu Mario Rajoy wakati wa zoezi hilo la kura ya maoni. Polisi waliovalia mavazi ya kivita, waliotumia virungu na risasi za mipira dhidi ya wapiga kura? Hasha, hilo hakuna anaeweza kulieleza mpaka watu wakalielewa."

Serikali ya Rajoy imeshindwa

Gazeti la Pforzheimer Zeitung linaandika: "Bila ya kujali matokeo ya kura ya maoni ya Katalonia yatakuwa ya aina gani, kimoja ni dhahiri , serikali ya mjini Madrid imeshindwa.Yeyote anaewapiga marungu na kuwafyetulia risasi za mpira raia wasiofanya fujo, anaonyesha hana anachokielewa. Kutokana na hali hiyo suala kama kura ya maoni ilikuwa kinyume na sheria au la, halina umuhimu mkubwa. Kwasababu kimaadili, mtu anaweza kusema wanaopigania kujitenga jimbo hilo wana hoja nzito na serikali kuu ya Uhispania ndio iliyowasaidia upande huo."

Muungano wa Jamaica utafanikiwa?

Gazeti la " Rhein-Zeitung" linamulika jukumu la kuundwa serikali ya muungano wa vyama vinne, CDU/ CSU, FDP na die Grüne inayojulikana kama serikali ya "muungano wa Jamaica". Gazeti linaandika: "Vyama ndugu vya CDU na CSU vitakapokubaliana pamoja na FDP na mwalinzi wa mazingira die Grüne, basi vitaipatia  jamii ya nchi hii msingi wa aina mpya  wa maisha, na kutilia maanani  kero za wengi. Pindi mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano yakifanikiwa siku za mbele kubuni sheria ya uhamiaji na pengine kuweka kiwango cha juu cha wahamiaji, hali hiyo inaweza kusaidia kurejesha amani katika jamii. Hilo linahusu masuala mengineyo pia ya kisiasa. Kinachohitajika ni ajenda ya mageuzi . Ajenda 2025. Kinachohitajika sio tuu usuluhivu wa Angela Merkel , bali pia mwenye kuona mbali mfano wa Willy Brandt na ndio, mwenye moyo wa kijasiri mfano wa Gerhard Schröder. Kitisho kilichopo ni kwamba muungano wa Jamaica hautoweza kuvumilia yote hayo."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com