1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni kuhusu ukarabati wa Camp Nou

4 Aprili 2014

Wanachama 164,000 wa Barcelona wanapiga kura Jumamosi (05.04.2014) ili kuamua kama klabu hiyo inapaswa kuendelea na mipango yake ya kuukarabati uwanja wa Camp Nou kwa kiasi cha euro milioni 600.

https://p.dw.com/p/1BcGX
Camp Nou Stadion in Barcelona Archiv
Picha: picture alliance/Back Page Images

Hata hivyo, mradi huo huenda ukagubikwa na wimbi la sifa mbaya linaloikumba bodi ya Barcelona katika miezi ya karibuni. Shirikisho la soka Ulimwenguni FIFA imeipiga marufuku ya miezi 14 klabu hiyo kuwasajili wachezaji baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka sheria za usajili wa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 18.

Habari hizo zimefuatia usajili wenye utata wa nyota wa Brazil Neymar mwaka jana ambao ulimfanya Sandro Rosell kujiuzulu kama rais wa klabu hiyo mwezi Januari mwaka huu na klabu hiyo ikatozwa faini kwa kukwepa kulipa kodi.

Rais wa zamani wa Barcelona Sandro Rosell katika kikao cha waandishi wa habari akitangaza kujiuzulu
Rais wa zamani wa Barcelona Sandro Rosell katika kikao cha waandishi wa habari akitangaza kujiuzuluPicha: Reuters

Rais mpya Josep Maria Bartomeu amejaribu kusisitiza kuwa umuhimu wa mradi huo una maana kuwa haupaswi kutumiwa kama kura ya maoni kwa bodi ya sasa, licha ya ukweli kwamba ilikataa kuitisha uchaguzi mpya wakati Rosell alijiuzulu.

Rosell anasema mradi huo utadumu kwa miaka 50 au 60 ijayo. Hata hivyo kumekuwa na upinzani kwa mradi huo kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa Barca ambao wanauona kama hatua ya kulifanya jina la klabu hiyo kuwa la kibiashara zaidi. Kati ya bajeti iliyopendekezwa ya euro milioni 600, euro milioni 200 zitatokana na mfadhili atakayeongezwa kwenye jina la kihistoria la Camp Nou. Ufadhili unaobaki utatokana na mkopo wa euro milioni 200 na sehemu ya mapato ya takribani euro milioni 500 ambayo klabu hiyo hutengeneza kila mwaka.

Mipango hiyo ni pamoja na kuweka paa kwenye uwanja huo mkubwa zaidi barani Ulaya na kuongeza uwezo wake wa idadi ya mashabiki, kutoka 90,000 hadi 105,000, pamoja na kujenga ukumbi mpya wa ndani unaoweza kutumiwa kwa shughuli chungu nzima, uwanja mpya wa timu ya pili ya Barca, eneo la kuegesha magari na ofisi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman