1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la ETA latangaza kusitisha mapigano

Josephat Nyiro Charo6 Septemba 2010

Wapiganaji wa ETA walitangaza kutofanya tena operesheni za mashambulio ili kusaidia kuanzisha mchakato wa demokrasia nchini Hispania. Serikali inasema haina imani na kauli hiyo

https://p.dw.com/p/P5AG
Waasi wa ETA wakitangaza kusitisha mapiganoPicha: AP

Katika tangazo lake la kusitisha mapigano, kundi la ETA halikusema kama linaachana kabisa na harakati zake za mapambano au kama hatua hiyo itadumu kwa muda tu. Kundi hilo lilitangaza uamuzi wake huo kwenye mkanda wa video uliotumwa kwa shirika la habari la BBC na gazeti linalochapishwa kila siku la Gara nchini Hispania, ambapo watu watatu waliokuwa wamejifunika nyuso zao na vitambaa vya rangi ya njano wakiwa wamekaa kwenye meza iliyozungukwa na bendera za eneo la Basque na nembo za kundi la ETA kwenye ukuta nyuma yao.

Sauti ya kike ilisika kwa lugha ya Kibaski ikisema, "Kundi la ETA linasisitiza tena kujitolea kwake kwa dhati kutafuta suluhisho la kidemokrasia kwa mzozo uliopo, ili raia wa eneo la Basque kwa misingi ya mdahalo na mashauriano waweze kupigia kura mustakabali wao kwa njia huru na ya kidemokrasia. "

Kundi la ETA ambalo linaorodheshwa na Marekani na Umoja wa Ulaya kuwa la kigaidi halijafanya shambulio lolote nchini Hispania tangu mwezi Agosti mwaka jana 2009. Katika miezi ya hivi karibuni kundi hilo limedhoofishwa na operesheni ya polisi kuwakamata viongozi wengi wa ngazi ya juu wa kundi hilo. Pia kulikuwa na mjadala mkubwa miongoni mwa wafuasi wa kundi hilo katika eneo la Basque kama huu sio wakati wa kukata tamaa na kuachana na vita vya kupigania uhuru wa eneo hilo.

Serikali ya Hispania hii leo imetoa taarifa ikilipuzilia mbali tangazo la kundi la ETA. Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo, Alfredo Perez Rubalcaba, amesema polisi wataongezea makali operesheni yao ya kuwasaka na kuwakamata waasi hao wa ETA wenye silaha. Waziri huyo aidha amesema tangazo la jana Jumapili halikutimiza takwa la jamii ya Basque na Wahispania kwa jumla, la kulitaka kundi la ETA lilaani na kuachana kabisa na machafuko.

Waziri Perez ameiambia televisheni ya taifa mjini Madrid kwamba anaamini licha ya tangazo la kundi la ETA kusitisha mashambulio yake, litaendelea na harakati zisizo halali kama vile kujilimbikizia silaha. Amesema kundi hilo limetangaza kusitisha mapigano kwa kuwa limekuwa dhaifu mno kiasi cha kutoweza kupanga mashambulio. Shambulio la mwisho la kundi la ETA lilifanywa mnamo mwezi Julai mwaka jana ambapo maafisa wawili wa polisi waliuwawa kwenye shambulio la bomu lililokuwa limetegwa ndani ya motokaa. Takriban wanachama 240 wa kundi la ETA wamekamatwa tangu mwaka 2008.

Kinachosubiriwa sasa ni kuona kama kweli kundi la ETA litasitisha mashambulio kama lilivyotangaza.

Mwandshi: Sulzmann, Daniel / Madrid (HR)/Josephat Charo

Mhariri: Abdul-Rahman