1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuna anayejali kuteketea kwa Somalia?

Mohamed Dahman25 Aprili 2007

Ni jambo lisiloyumkinika kwa Eritrea kutuma wanajeshi wake katika mji mkuu wa Somalia uliokumbwa na mapigano licha ya kuwepo kwa madai ya Marekani kwamba serikali ya Eritrea inaunga mkono waasi wanaopambana na vikosi vya Somalia na vile vya Ethiopia katika mji mkuu wa Mogadishu.

https://p.dw.com/p/CHFW
Wapiganaji wa Mogadishu wakipambana na vikosi vya Ethiopia
Wapiganaji wa Mogadishu wakipambana na vikosi vya EthiopiaPicha: AP

Kwa mujibu wa Roland Marchal mtafiti katika Kituo chenye makao yake mjini Paris Ufaransa cha Masomo ya Kimataifa na Utafiti wakati ni jambo la kuaminika kuwa serikali ya Eritrea inaunga mkono waasi wanaopambana na hasimu yake Ethiopia huko Mogadishu kuingilia kati kijeshi kwa Eritrea nchini Somalia ni jambo linaloonekana kuwa haliwezekani.

Marchal anasema serikali ya Eritrea yumkini kabisa ikawa inawapa mafunzo vikosi vya waasi nchini Eritrea na kuwapa waasi hao msaada wa vitu na vifaa uwezekano wa kujiingiza kijeshi katika mji mkuu huo wa Somalia kutakuwa kugumu sana au iwapo itafanya hivyo basi itakuwa kwa kiwango kidogo sana.

Marekani hapo Jumatatu imeishutumu Eritrea kwa kupalilia moto unaowaka wa mzozo wa Somalia kwa kugharamia na kuwapatia silaha na mafunzo waasi wanaopambana na vikosi vya serikali ya Somalia vikisaidiwa na vya Ethiopia.

Ethiopia iliingilia kati nchini Somalia kwa baraka za kimya kimya za Marekani hapo mwezi wa Desemba kusaidia kuutimuwa Muungano wa Mahkama za Kiislam uliokuwa umedhibiti karibu nchi nzima.Tokea wakati huo vikosi vya Ethiopia na waasi mjini Mogadishu wamekuwa wakipambana kwa vifaru,mizinga na silaha nyengine nzito mapigano ambayo yamegharimu zaidi ya maisha ya watu 1,000 ambapo 256 pekee wameuawawa katika kipindi cha wiki moja iliopita na kuwalazimisha wengine maelfu kwa maelfu kukimbia nyumba zao.

Kuongezeka kwa umwagaji damu na mashambulizi mazito ya mabomu ya Ethiopia kumezusha shutuma za kimataifa ikiwa ni pamoja na kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon ambaye amelaani kutumiwa ovyo kwa silaha nzito dhidi ya maeneo ya kiraia bila ya kujali sheria ya kimataifa ya ubinaadamu.

Kwa upande mwengine inaonekana kwamba mkakati wa Ethiopia kutokomeza uasi umeanza kuzaa matunda kwa waasi kuanza kuishiwa na silaha kwa vile wanajeshi wa serikali wakishirikiana na wale wa Ethiopia wamedhibiti njia zote za kuingia Mogadishu kuanzia viwanja vya ndege na hadi zile za barabara.

Inaonekana kama kwamba suluhisho la kijeshi ndio linalofanya kazi leo hii na watalaamu wa mataifa ya magharibi wanakubali kwamba Ethiopia iko Somalia kwa kudumu.

Umwagaji damu na mateso yalioko Somalia yumkini yakawa mabaya kabisa kushuhudiwa katika kipindi cha muongo mmoja lakini habari zake ni za nadra na hiyo inatokana na sababu mbali mbali kuanzia na kuchoshwa na migororo ya Afrika,kugawika kwa diplomasia ya kimataifa juu ya mzozo huo na kukata tamaa vita vyenye kuuwa raia vimeshindwa kuvuta nadhari ya dunia na kuamsha wale wenye sauti kuu duniani kuchukuwa hatua.

Kiongozi wa jopo moja la watu mashuhuri nchini Somalia ambaye amekataa kutaja jina lake kwa hofu za usalama amesema kuna maafa makubwa yanayotokea Mogadishu lakini kutokana na dunia kukaa kimya utadhani kwamba ni X’masi.

Mogadishu ni pahala pa hatari sana hususan kwa waandishi wa habari wa kigeni.Taswira za kufadhaisha ziko kila mahala...maiti zimetapakaa barabarani,majengo yalioharibiwa,watoto wachanga waliojeruhiwa,wakimbizi chini ya miti,kumbi za hospitali ziliorowa damu na kuhanikiza kwa vilio.

Hayo yamekuwa hayawezi kuonekana nje kwa sababu ya hatari ya kuchukuwa filamu hizo na kuwepo kwa wachukuaji picha wachache.

Wasomali wanaona pia kwamba wanasiasa wenye uwezo wa kuchukuwa hatua hawalizungumzii hilo pengine kwa kuamini kwamba Wasomali wamejitakia hayo wenyewe na inastahili yawakute.