1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu ya miaka 70 ya bomu la nyuklia Nagasaki

9 Agosti 2015

Wahanga wa bomu la nyuklia wa mji wa Nagasaki wameikosowa hatua ya Japan ya kutanuwa dhima yake ya kijeshi nchi za nje wakati ikiwa katika kumbukumbu ya miaka 70 ya shambulio hilo la Mareakani Jumapili (09.08.2015.

https://p.dw.com/p/1GCP4
Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe wakati wa kumbukumbu ya miaka 70 ya shambulio la bomu la atomiki kwa mji wa Nagasaki . (09.08.2015)
Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe wakati wa kumbukumbu ya miaka 70 ya shambulio la bomu la atomiki kwa mji wa Nagasaki . (09.08.2015)Picha: Reuters/T. Hanai

Katika ibada ya kumbukumbu hiyo iliofanyika katika Bustani ya Amani mjini humo Sumiteru Taniguchi muhanga wa bomu hilo mwenye umri wa miaka 86 ameshutumu miswada ya usalama ya serikali kwa kwenda kinyume dhidi ya matakwa ya wahanga ambao kwa Kijapani wanajulikana kama "hibakusha".

Taniguchi amekaririwa akisema "Muswada huu wa usalama ambao serikali inataka kuupitisha utapelekea vita." Ameongeza kusema "Ni jaribio la kutenguwa harakati za kupiga marufuku silaha za nyuklia na matakwa yanayoshikiliwa na kutekelezwa na hibakusha na umma mkubwa wa watu wa mataifa mbali mbali wenye shauku na amani.Hatuwezi kulikubali jambo hili."

Kumbukumbu hii inafanyika wakati bunge la Japani likijadili muswada wa sheria ambao unaweza kuliruhusu jeshi kupigana vita nchi za nje kwa mara ya kwanza tokea kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Ibara ya tisa ya katiba ya Japani inayokana vita inapiga marufuku matumizi ya nguvu kusuluhisha mizozo ya kimatafa.

Hali ya mzozo

Katibu Mkuu wa Baraza la Wahanga wa Bomu la Nyuklia wa Nagasaki Hirotami Yamada amesema serikali ina shauku ya kiwezesha nchi hiyo kupigana vita.Yamada ambaye alipoteza wazazi wake na ndugu zake watatu katika shambulio hilo anasema manusura wa bomu hilo la nyuklia wanaona kuna mzozo.

Wananchi wa Japani wakati wa kumbukumbu ya miaka 70 ya shambulio la bomu la atomiki kwa mji wa Nagasaki . (09.08.2015)
Wananchi wa Japani wakati wa kumbukumbu ya miaka 70 ya shambulio la bomu la atomiki kwa mji wa Nagasaki . (09.08.2015)Picha: Reuters/T. Hanai

Nagasaki ina makundi matano ya manusura ambayo yalikuwa yamegawika lakini hivi sasa yote yameungana kuwa kitu kimoja na kupinga vikali muswada huo wa sheria.

Wakati wa kumbukumbu hiyo Waziri Mkuu wa Japani Shizo Abe amesema serikali yake itaendelea kushikilia kanuni za Japani za kupinga silaha za nyuklia.

Waziri Mkuu huyo amekosolewa kwa kuotaja sera hiyo katika hotuba yake hapo Alhamisi kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 7o ya kudondoshwa kwa bomu la nyuklia kwa mji wa Hiroshima.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Japani (NHK)takriban watu 6,000 wamehudhuria ibada ya kumbukumbu hiyo hapo Jumapili katika Bustani ya Amani ya Nagasaki akiwemo balozi wa Marekani nchini Japani Caroline Kennedy,msaidizi waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwa masuala ya Udhibiti wa Silaha na Usalama wa Kimataifa Rose Gottemoeller na wadiplomasia kutoka nchi nyengine 74.

Maafa ya mabomu hayo

Washiriki hao walikaa kimya kwa dakika moja kuanzia saa tano na dakika mbili wakati hasa bomu hilo la atomiki lilipodondoshwa kutoka anga ya Nagasaki.Bomu hilo lilikuwa la pili wakati vita vikuu vya pili vya dunia vilipokuwa vikifikia mwisho na kusababisha vifo vya watu 74,000 na kujeruhi wengine idadi kama hiyo katika mji huo ambao wakati huu ulikiwa na idadi ya watu 240,000.

Sanamu ya Amani katika Bustani ya Amani Nagasaki.
Sanamu ya Amani katika Bustani ya Amani Nagasaki.Picha: Reuters/T. Hanai

Siku tatu kabla ya hapo maelfu kwa maelfu ya watu waliuwawa katika kipindi cha sekunde chache kutokana na shambulio la bomu la nyuklia kwa mji wa Hiroshima.

"Kwa maslahi ya Nagasaki na kwa maslahi ya Japani inabidi tusibadili kanuni ya amani ambayo kwayo tumevikana vita" Hilo lilikuwa tamko la Meya wa Nagasaki Tomihisa Taue aliyoitowa katika kumbukumbu hiyo akigusia ibara ya tisa ya katiba.

Mara tu baada ya kuripuliwa kwa mabomu hayo wahanga walikuja kuteseka na kipindu pindu,nywele zao zilikuwa zikiwatoka na kuvuja damu puani.Hayo anayakumbuka vuzuri muhanga Michiko Yagi mwalimu mkuu wa zamani wa shule ya serikali katika mji wa Nagasaki.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa

Mhariri : Caro Robi